Binti aliyemchapa, kumng’ata  Profesa afunguka mazito

NA ROBERT JULIUS

BINTI aliyekuwa amefungwa na nguvu za giza na kuwa tishio kwa familia ya Prof. Emmanuel Mjema, msharika wa Kunduchi Beach jijini Dar es Salaam, amefunguka mazito juu ya mambo yaliyokuwa yanamsababishia kufanya vitendo hivyo.

Binti huyo (jina tunalihifadhi), alikuwa tishio kwenye familia ya Profesa huyo na ukifika wakati wa maombi alikuwa akipata nguvu za kuwachapa fimbo wanafamilia, kuwang’ata na kuwasababishia majeraha, kwa sababu maombi yalikuwa yanaharibu mipango iliyokuwa imepangwa dhidi yake.

Binti huyo anatoka katika imani nyingine ambapo kila mwaka mara mbili, lazima watu wa ukoo wake wafe kwa kutolewa kafara ili kutimiza maagano ya miungu yao.

Mwaka huu ilikuwa zamu yake ya kutolewa kafara, hivyo vita vilihamishiwa kwa familia ya Prof. Mjema ambayo ilikuwa kikwazo kwa kutomwachia kurudi kwao Manyara.

Akizungumza na UPENDO, binti huyo alisema hakuwa akijitambua wakati anawachapa na kuwang’ata wanafamilia kwani alikuwa anatawaliwa na nguvu nyingine.“Sikuwa najitambua, nakumbuka tu siku moja wakati wa maombi nilianza kujisikia vibaya, nilikuwa nasikia kizunguzungu na kichwa kinaniuma,” alisema.

Katika maelezo ya awali yaliyotolewa na Prof. Mjema, binti huyo alianguka wakati wa maombi na mapepo yaliyokuwa ndani yake yalianza fujo na kufikia hatua ya kuwang’ata wanafamilia ‘yakiwalazimisha’ kumkana Yesu.

Prof. Mjema ambaye anaishi na binti huyo kwa muda wa takribani miezi sita, aliliambia UPENDO kuwa msichana huyo alitakiwa akatolewe kafara huko kwao, hivyo vita kubwa ilikuwa kati ya waliokuwa wanataka binti arudi nyumbani dhidi ya familia yake ambayo iligoma kumwachia.

Profesa huyo alisema wakati wakiwa kwenye maombi, malaika alikuwa akijidhihirisha kupitia binti huyo kueleza kila kilichositirika katika ukoo wa binti huyo mambo ambayo  familia yake haikuwa ikiyafahamu.Pia alikuwa akiwaambia mambo yote yatakayotokea baadaye juu ya vita iliyokuwa ikiwakabili. 

Kupitia udhihirisho huo, ndipo walipotambua kuwa binti huyo anatakiwa kwa ajili ya kafara, na akawaambia kila kitu watakachokutana nacho.Wakati vita ilipokuwa kubwa na kuanza kushambuliwa, malaika aliwaambia wasikemee bali wamsifu Mungu kwa kumwimbia, jambo ambalo walilitii kwa moyo mmoja licha ya kuumizwa.

Kwa mujibu wa Prof. Mjema, malaika huyo aliwaambia kuwa mkuu wa ukoo ambaye alikuwa anasimamia masuala yote ya kutoa kafara atakufa na siku ya Februari 29 atakuwa kaburini.Familia hiyo iliendelea kumsifu Mungu katika kipindi chote cha takribani mwezi mmoja na nusu licha kuchapwa na kung’atwa.

Ukoo wa binti huyo una kawaida ya kutoa kafara kila miezi ya Aprili na Juni kila mwaka na huo ni mkataba ambao ulifanywa kuanzia vizazi vinne vilivyopita.Prof. Mjema anasema kuwa mauti ilianza kumwandama binti huyo tangu akiwa tumboni mwa mama yake, kwa sababu wakati wa ujauzito alijaribu kuutoa mara tatu lakini ikawa inashindikana.

“Wakati akiwa mdogo walijaribu kumtoa kafara ikashindikana, lakini mambo yake yalikuwa mabaya zaidi siku alipobatizwa, kwani hapo ndipo alianza kusakamwa zaidi ili afe kwani amekiuka masharti ya ukoo,”alisema Profesa Mjema.Kutokana na kuwa nguvu za kichawi nyuma ya binti huyo Prof. Mjema alisema wakiwa kwenye maombi walikuja watu kutoka ukoo huo kwa njia ya kichawi kupambana na familia yake lakini walishindwa.

Alisema  baada ya kundi moja la kichawi kutoka ukoo wa binti huyo kushindwa, lilitumwa lingine, hadi siku moja malaika alipojidhihirisha tena na kuwaambia vita hiyo wamwachie yeye na kwamba binti huyo aliletwa katika familia hiyo kwa kusudi maalumu ili kizazi chao wapate kukombolewa.“Walikuwa wanachukua ufahamu wake na kumuwekea mapepo ya kung’ata na kufanya uharibifu wa vitu, lakini kumbe lengo lilikuwa ni tumchoke tumfukuze, ili tumrudishe kwao,” alisema Prof. Mjema.

Prof. Mjema alisema kuwa kuna wakati malaika alikuwa anajidhihirisha kupitia binti huyo (kwa mujibu wa maelezo yake, malaika alipokuwa akijidhihirisha kupitia binti huyo hata sura ilikuwa inabadilika, tofauti na pale anapokuwa anatumiwa na pepo).Malaika aliwaambia kuwa imani yao lazima ijaribiwe na kuwaambia kuwa hata Mitume walijaribiwa. Alisema Malaika aliwapa taarifa  za kifo cha mkuu wa ukoo na baadaye walithibitishiwa baada ya binti huyo kutumiwa ujumbe wa simu kuhusu kifo hicho. Aliwaambia kuwa atakapozikwa ndipo ufahamu wa binti huyo utarejea. 

Alieleza kuwa baada ya kifo cha mzee huyo wa ukoo chumba chake cha uganga kitawaka moto, na kila kitu kikateketea vikiwamo vibuyu kupasuka, lilionekana karatasi nyeupe limeandikwa 'imekwisha.' 

Alisema huko Babati baada ya chumba cha kiganga kuteketea, Dar es Salaam binti alipiga kelele kwa sauti kubwa akisema ‘imekwisha’ na kwamba baada ya maziko huko Babati, binti huyo alirejeshewa ufahamu wake kwani alikuwa haelewi alipo wala alichokuwa anafanya. “Siku aliporudishwa ufahamu alianza kutuuliza hapa tuko wapi,” alieleza Prof. Mjema.

WASHARIKA WAZUNGUMZA

Baadhi ya washarika wa Kunduchi Beach waliomsikia Profesa Mjema akitoa ushuhuda walisema kuwa ushuhuda huo umewaimarisha kwa kiwango cha juu.

Baraka Nickson alisema kuwa watu wanapaswa kuamini kuwa Yesu Kristo yupo na anatenda. “Nampongeza Prof. Mjema kwa kupambana na vita hivyo kwa sababu ule ushuhuda umewajenga watu na vita siyo vyetu ila ni vya Bwana,” alisema.

Edmund Lweikiza, alisema ameona jinsi Mungu anavyofanya kazi kwa njia za ajabu. “Tunatakiwa kuwa watulivu na wavumilivu tunapohudumia watu waliofungwa na nguvu za giza,” alisema Lweikiza na kuongeza kuwa watu watambue kuwa wanapoona mtu anatumiwa na mapepo wajue kuwa na Mungu anaweza zaidi kuwatumia watu.“Shetani anatumia watu na Mungu anatumia watu, kwa hiyo ni suala lako kutambua kuwa hapa ni nani anayesema,” alisema.

Evelyne Songambele alisema kuwa aliguswa kwa kiwango cha juu na ushuhuda huo na kuwataka watu ambao walikuwa wamemuacha Mungu wamrudie. Alisema Prof. Mjema aliamua kushikamana na Mungu bila kuogopa. Naye Jesca Brighton alisema kwa jinsi Profesa alivyokuwa anaongea na jinsi alivyoonesha majeraha aliyoyapata mwilini alishangaa sana.

“Kwa kweli Mungu ni wa ajabu kitendo alichokifanya Profesa ni cha kumtukuza Mungu na kumtangaza Kristo ili kila mtu apate kuamini kuwa Mungu yupo,” alisema.Msharika mwingine, Emma Mgina alisema ushuhuda huo ulimsisimua na kueleza kuwa ukimsikia mtu anapotoa ushuhuda kama ule unaweza kusema labda ni uongo, ukaanza kujiuliza kwani hayo makovu huko usoni amefanyaje na mke wake.“Ule ushuhuda umenijenga kumbe hakuna uchawi wala uganga mbele ya jina la Yesu, uchawi ni kitu gani?” alihoji na kuongeza kuwa hata akitembea anatembea kifua mbele kwa sababu anajua kuwa ana Yesu.“Nawaambia wasioamini wasome Biblia wailewe,” alisema Mgina.Profesa Mjema alisema kuwa atatoa sadaka ya shukrani ya pekee Jumapili Machi 15 kutokana na Mungu kumshindia vita hiyo kubwa.

Vilevile Profesa huyo alisema kuwa atakwenda na binti huyo nyumbani kwao Manyara mwezi Juni mwaka huu ili akaelezee kila kitu kilichotokea. Alisema kuwa huo utakuwa mwanzo wa kuvuna watu wengi kumfuata Yesu.

This news is from UPENDO, the weekly newspaper of ELCT Estern and Coastal Diocese.
Follow us on Facebook , Instagram and Youtube.