Mbezi Ndumbwi: Kutoka  Mtaa, Usharika sasa kumiliki Shule ya Awali

NA ARAFUMANDE MUNUO

UNAPOZUNGUMZIA mitaa iliyozaliwa na  kuwa Usharika katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) ya KKKT, hutaacha kuuzungumzia Usharika wa Ndumbwi wa Jimbo la Kaskazini, ambao ni uzao wa Usharika wa Mbezi Beach wa jimbo hilo.

Usharika wa Ndumbwi ninaweza kuufananisha na mtoto mchanga aliyezaliwa na kulelewa na wazazi wake kisha kuondoka  nyumbani kwenda kujitegemea na kuanza kupata mafanikio huku wazazi wake wakiyashuhudia, pengine mafanikio hayo wao kwa sehemu hawakuyafikia.Ninayasema haya kwa sababu Ndumbwi ambao ni uzao wa Usharika wa Mbezi Beach leo hii baada ya kuanza kujitegemea kwa maana ya kuondokana na utegemezi kutoka kwa Baba umeweza kuanzisha shule ya awali ya watoto, muda mfupi tu baada ya kupewa kibali cha kuanza maisha mapya.

Usharika wa Ndumbi ni moja kati ya Sharika zilizobarikiwa rasmi kuwa sharika, baada ya kupita katika kipindi cha kuwa Mtaa kwa takribani miaka 15 na kufunguliwa kuwa Usharika mwaka 2018 baada ya kupitishwa na Halmashauri Kuu ya DMP mwaka 2017 kutokana na kukidhi vigezo vya kuwa Usharika.Usharika huo kama zilivyo sharika nyingine ulipita katika michakato mbalimbali mpaka kuwa hapo ulipofikia sasa ukiwa na mafanikio lukuki ya kiroho na kimaendeleo kwanza kuwa na jengo zuri la Ibada la kuabudia  na jengo la kisasa la watoto wa shule ya Jumapili.

Si hivyo tu, Usharika huo kwa sasa ni miongoni mwa Sharika chache za DMP, zinazomiliki Shule  ya awali. Ndumbwi imefanikiwa kuanzisha shule hiyo ambayo imeanza rasmi mwaka huu 2020 iliyopewa jina Galilee Day Care English Medium.

MCHUNGAJI KIONGOZI

Akielezea uanzishwaji wa shule hiyo ya awali, Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo,  Christowelu Gabriel Mande, alisema uanzishwaji wa shule hiyo ulitokana na mawazo ya washarika.Baada ya kuona jengo la watoto wa shule ya Jumapili lenye ghorofa tatu lililopo usharikani hapo lisitumike kwa hasara kwa wiki nzima ndipo wakaazimia kupitia Mkutano Mkuu wa Usharika wa mwaka 2017 na 2018 kuanzisha shule hiyo hasa kutokana na eneo uliopo usharika huo kutokuwa na shule ya watoto.

“Washarika pia waliona kuanzishwa kwa shule hiyo kutausaidia usharika kupata maendeleo ikiwemo kwenye suala la uchumi.”Mchungaji huyo alibainisha kuwa uanzishwaji wa shule hiyo umefuata taratibu zote za Wizara ya Elimu ikiwemo kukagua madarasa kwa ajili ya watoto na walimu wenye vigezo ambao wanatambuliwa na Tamisemi.

“Ili kukwepa mwingiliano wa uongozi tuliunda bodi ya ndani ya shule yenye wajumbe sita inayosimamiwa na Kamati ya Malezi ya Usharika pamoja na Kamati ya Elimu ambao ndio watakaosimamia shule hiyo.”Akizungumzia mipango mingine ya Usharika kwa mwaka huu, alisema ni kuboresha Ibada zao za kila Jumapili kwa kutoa mafundisho sahihi pamoja na huduma bora za kiroho.

Kadhalika, kuimarisha mafundisho kwa kuwa na semina ya wiki moja kila mwezi yenye lengo la kuwajenga Wakristo kiimani.Mchungaji Welu, pia alieleza kuwa mwaka huu wamezindua kampeni maalumu kwa vijana iitwayo The Season and Reason of Worship Fellowship ambayo itakuwa ikifanyika kila mwezi siku ya Jumapili mchana lengo likiwa ni kuwajenga vijana katika maadili mema ya kumjua Mungu.

Kwa upande wa kinamama, ameeleza kuwa wameanzisha kikundi cha vikoba ambacho hicho kimetumika kuwakusanya kinamama mtaani na kuwaleta kanisani hasa kikilenga kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo kama wanawake ambao hasa ndio wasimamizi wa familia.

Kwa upande wa watoto, alisema wameendelea kupeleka walimu wa Shule ya Jumapili kwenye mafundisho yanayotolewa na DMP katika Chuo cha Maneromango lengo hasa likiwa ni kuwajengea misingi bora ya kutoa mafundisho sahihi kwa watoto ambapo mpaka sasa jumla ya walimu wanane wameshapatiwa mafunzo hayo.

MAENDELEO YA USHARIKA

Kwa upande wa maendeleo ya Usharika, mchungaji alieleza kuwa kwa sasa wameshaanza ukarabati wa madhabahu ya kisasa ambayo itagharimu shilingi milioni 25 ambayo wamekusudia mpaka Juni mwaka huu wawe wamekamilisha.Pia, alieleza kuwa wanakusudia kunakshi jengo lao la Ibada na kulifanya liwe katika mwonekano mzuri na wa kisasa zaidi, mipango ambayo ameeleza kuwa mpaka mwishoni mwa mwaka huu itakuwa imekamilika.Sambamba na hili pia alieleza mipango mingine ni kuboresha makazi ya watumishi.

Mchungaji huyo alisema anamshukuru Mungu yote hayo yanafanywa kwa nguvu za Washarika wenyewe ambao ameeleza kuwa wamepewa elimu ya kujiungamanisha na madhabahu ili Mungu ashughulike na haja ya mioyo yao kupitia sadaka.

NDUMWI ILITOKEA WAPI?

Usharika wa Mbezi Ndumbwi, ulianza kama mtaa uliokuwa chini ya Usharika wa Mbezi Beach Septemba, 2005. Kuanzishwa kwa mtaa huo kulitokana na wazo la Wakristo Walutheri waliokuwapo eneo hilo na ulichangiwa na umbali uliokuwapo kutoka eneo lililopo Kanisa kwa sasa hadi usharikani Mbezi Beach.Inaelezwa kuwa wakati wa mvua, Mto Ndumbwi ulijaa maji na Wakristo walishindwa kabisa kupita kwenda kuhudhuria Ibada katika Usharika wa Mbezi Beach.

Kutokana na changamoto hiyo, familia za Wakristo Walutheri walimwomba mzee Kundansari Mwasha ambaye alikuwa Mzee wa Kanisa Usharika wa Mbezi Beach kwa wakati huo, kuwasaidia kuona namna ya kuwa na ibada katika maeneo yao.Mzee Kundansari Mwasha kwa kushirikiana na Mwinjilisti Lazaro Nsanya (kwa sasa ni Mchungaji) walisaidia kumpata Mwinjilisti Jane Kamugisha (ambaye kwa sasa ni Mchungaji), ndipo walipoanza ibada rasmi nyumbani kwa Stanley Magawa. 

Ibada ya siku ya kwanza ilihudhuriwa na Wakristo Walutheri watu wazima 26 na watoto 25. Baada ya kuona idadi ya washarika inaongezeka siku hadi siku uongozi wa Mtaa ulianza mchakato wa kutafuta eneo kubwa la kuabudia, ndipo Agosti 2006 walifanikiwa kupata eneo lililojengwa Kanisa kwa sasa kwa thamani ya shilingi milioni  22 na kuanza kuabudu katika kiwanja hicho mwezi huohuo.

Kufikia Desemba 2006 washarika hao  walikuwa tayari wamekamilisha ununuzi wa eneo hilo na kwa kuanzia, lilijengwa jengo dogo la miti na kupaua kwa bati; na baadaye 2007-2008 walijenga jengo la matofali lililozinduliwa sambamba na uzinduzi wa Mtaa, Aprili mwaka 2012 na Askofu Dk. Alex Malasusa.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa DMP pamoja na wageni kutoka Kanisa la Kilutheri nchini Sweden ambao walifika katika Dayosisi hiyo kwa lengo la kuendeleza uhusiano katika kuujenga mwili wa Kristo.

CHIMBUKO LA NDUMBWI

Akizungumza na Gazeti hili, Kiongozi wa Serikali za Mitaa eneo la Ndumbwi Musa Mwazembe, alieleza kuwa  neno Ndumbwi lilianza kama utani sababu lilianzishwa na  watoto wa Kimakonde waliokuwa wakikaa eneo hilo miaka kati ya 1920- 1930. Watoto hao walikuwa wanakaa ng’ambo ya barabara eneo la NSSF ambalo lipo Barabara ya Bagamoyo.

Alieleza kuwa watoto hao walikuwa wakicheza katika eneo hilo, kutoka upande wa pili wa barabara. Eneo hilo lilikuwa na mfereji wa mto ambao ulikuwa na kibwawa. “Walipokuwa wanakuja kucheza wanarusha mawe kwenye maji maji yanalia ndumbwiii… ikawa wakiwa wanakwenda upande huo wanasema tunaenda kule panapolia ndumbwiiii… ndipo jina lilipoanzia na kuitwa Ndumbwi”

Aliongeza kuwa mto huo “Uliingiliwa na wavuvi waliokuwa wanakuja kukata miti wanasema tunaenda ndumbwi hao ndio waliopaisha zaidi jina la Ndumbwi. Wenyeji kabisa ni Wamakonde.”

MAFANIKIO

Idadi ya Washarika imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka watu wazima 26 na kufikia watu 800, watoto wa shule ya Jumapili 25 na kufikia 250. Usharika huo una nyumba ya mtumishi na ofisi mbalimbali. Pia, umefanya upanuzi wa jengo la Ibada kutoka uwezo wa Washarika kukaa 400 mpaka kufikia 750.

Mafanikio mengine usharikani hapo ni pamoja na jengo la watoto lenye madarasa matatu yenye uwezo wa kuchukua watoto 60 kila moja. Mwinjilisti wa Usharika huo, Selestine Umela, alieleza kuwa hii inasaidia kuwatenga watoto kutokana na umri wao; na kuwafundisha.  Aliongeza kuwa jengo hilo lina ofisi mbalimbali za watumishi na vikundi.

VIKUNDI

Usharika wa Ndumbwi una vikundi vitano vya uimbaji; Kwaya ya Vijana, Kwaya Kuu, Kwaya ya Kinammama, Kwaya ya Uinjilisti na Kwaya ya Tarumbeta.

KWAYA KUU

Kwaya Kuu ya Usharika huo ilianzishwa rasmi mwaka 2006, ikiwa na waimbaji 20 na waimbaji wote wakati huo walikuwa wanawakeBaada ya muda mfupi tangu kuanzishwa mtaa huo, kwaya hiyo iliongezeka idadi ya waimbaji na kufikia 34 na mpaka sasa  waimbaji 24, wengine wamehama Usharika kwa sababu ya makazi na shughuli za kiuchumi.

Kwaya hiyo imefanikiwa kurekodi albamu ya kwanza audio mwaka 2014  na albamu ya pili ya video DVD mwaka 2017, licha ya mafanikio ya kurekodi kwaya hio pia imefanikiwa kupeleka Injili ndani na nje ya usharika huo ikiwemo kushiriki matukio mbalimbali ya kidayosisi ikiwemo mashindano ya uimbaji.

Kwaya hiyo ina maono kadhaa ikiwemo kuboresha uimbaji, kuongeza albamu nyingine,  kukuza na kuimarisha shughuli za kiroho, pamoja na kuanzisha miradi ya itakayoiwezesha kukabiliana na changamoto za kifedha.

KWAYA YA KINAMAMA

Kwaya hii ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na waimbaji 10, baadaye idadi iliongezeka na kufikia waimbaji 17.Kwaya ya Kinamama Ndumbwi ina maono kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na kuzindua Audio CD mwaka huu. Maono mengine  ni kuanzisha miradi mbalimbali ya kuwaongezea kipato kama kikundi  ili kuweza kuendesha shughuli za kwaya ikiwemo kuwatembelea wahitaji.

MAFANIKIO

Kwaya hiyo imefanikiwa kurekodi nyimbo 10 katika mfumo wa audio mwaka 2019, mbali na mafanikio hayo kwaya hiyo inakabiliwa na changamoto  ya ukosefu wa fedha uliowasababishia kushindwa kuzindua Audio CD yao pamoja na uchache wa waimbaji.

KWAYA YA VIJANA

Kwaya ya Vijana Ndumbwi, ilianzishwa mwaka 2015, ikiwa na waimbaji 10. Kwaya hiyo ilikuwa na kufikia waimbaji 40 kwa muda mfupi.

MAFANIKIO

Vijana Ndumbwi, wamefanikiwa kurekodi albamu moja ya Audio,  wamefanikiwa pia kuhudumu katika ibada mbalimbali za Sharika na mitaa ya DMP pamoja na matukio ya Usharika wao.

Palipo na mafanikio, hapakosi changamoto. Kwaya hii ina changamoto ya ukosefu wa mwalimu, mahudhurio hafifu ya waimbaji kutokana na waimbaji wengi asilimia kubwa kuwa ni wanafunzi wakiwamo viongozi wa kwaya hiyo.

Kama zilivyo kwaya nyingine za Usharika huo, hiyo inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na mradi wa kusaidia kundi.

Kwaya ya Vijana Ndumbwi ina maono mbalimbali ikiwemo kuongeza albamu nyingine katika mfumo wa DVD, kuongeza kiwango cha uimbaji kwa waimbaji wake pamoja na kukuza watu kiroho.

Kwaya hiyo ina mipango kadhaa ikiwemo kumtafuta mwalimu kwa msaada ya Kamati ya Malezi na wanakwaya, kukusanya wanakwaya wapya na kuwasaidia waliorudi nyuma katika huduma pamoja na kuanzisha mradi  wa kikundi.

 KWAYA YA UINJILISTI

Kwaya ya Uinjilisti New Jerusalem Ndumbwi, ilianzishwa mwaka 2009 ikiwa na idadi ya waimbaji 9. Mpaka sasa ina waimbaji 19.Kwaya hii ilianzishwa kwa malengo ya kuhubiri injili kwa njia ya uimbaji, kutoa huduma ya maombi na maombezi ikiwemo kutoa faraja kwa wagonjwa na wenye matatizo mbalimbali ndani na nje ya Usharika.

MAFANIKIO

Kwaya hii  imefanikiwa kurekodi Audio CD mwaka 2011, iliyobeba jina la Jihadharini na imefanikiwa kufanya huduma za Kiinjilisti pamoja na kuwagusa watu wenye mahitaji mbalimbali.

CHANGAMOTO

Uinjilisti Ndumbwi  inakabiliwa na ukosefu wa fedha uliosababisha ishindwe kurekodi albamu ya pili  kwa njia ya audio  na video kwa albamu ya kwanza.Kwaya hii pia inakabiliwa na uhaba wa vyombo vya muziki  hivyo kushindwa kuimba katika viwango na ubora unaostahili.Vyombo hivyo ni pamoja na kinanda, ngoma, vinasasauti na spika ambazo zitawawezesha si tu kutoa huduma usharikani bali katika maeneo mengine nje ya usharika wao.

Kwaya hii pia inakabiliwa na upungufu wa waimbaji unaosababishwa na changamoto mbalimbali za kimaisha pamoja na wengine kuhamishwa vituo vya kazi.

WAUMINI WAZUNGUMZIA USHARIKA WAO

Akizungumza na Gazeti hii usharikani hapo, Reymond Kawesa, alieleza kuwa amekuwa muumini wa usharika huo tangu 2012  ukiwa mtaa. Anajivunia kuwepo mahali hapo kutokana na huduma nzuri za kiroho zinazotolewa usharikani hapo  na kwa namna usharika huo unavyoendelea kukua siku hadi siku.

“Naona fahari  kuwepo mahali hapa huduma zote tunazozihitaji tunazipata.”Ametoa wito kwa waumini wa madhehebu mbalimbali waliopo katika eneo hilo kufika usharikani hapo kuona namna wanavyomuabudu Mungu katika roho na kweli.

Esteria  Msoso, alieleza kuwa tangu alipofika katika Usharika  huo anaridhishwa na huduma zinazotolewa, waumini wanapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wao wa ibada na kusikilizwa pale wanapohitaji msaada mbalimbali  ikiwemo huduma za maombi na maombezi.“Tunapata huduma nzuri za kiroho, Mungu yupo mahali hapa anatuhudumia, watu waache kutangatanga katika makanisa wamwamini Mungu walipo anawasikia.”

Naye Asnath Julius alimweleza mwandishi wa gazeti hili kuwa  “Nipo katika usharika huu tangu mwaka 2013 ukiwa mtaa, tunamtukuza Mungu ametupa watumishi wenye hofu  ya  Mungu,  unapofikwa na shida unapata msaada wa ushauri. Tuna huduma ya maombi na maombezi usharikani kwetu, tuna ibada za kila siku asubuhi,  katika yote haya tunamuona Mungu akituhudumia kupitia watumishi tulionao. Ndumbwi ya sasa si kama ya miaka mingine.” 

WATUMISHI WALIOPO

Ndumbwi ina watumishi watano akiwamo Mchungaji Kiongozi  Christowelu Gabriel Mande, Mchungaji Lidya Mwimi (aliyeko Zanzibar), Mwinjilisti Selestine Gerald Umela, Mwinjilisti Sekela Ezekia Mwaikenda na Mtunzahazina Gerald Kashagile.

This news is from UPENDO, the weekly newspaper of ELCT Estern and Coastal Diocese.
Follow us on Facebook , Instagram and Youtube.