ASKOFU wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa ametoa rai kwa Sharika za Dayosisi hiyo kuzidi kutambua umuhimu wa kutunza Mitaa. Kuna maeneo mengi ambayo bado watu hawajasikia habari za Yesu.

Askofu Dk. Malasusa aliyasema hayo wakati wa Ibada ya kufungua Usharika wa Changanyikeni, iliyofanyika Jumapili iliyopita Usharikani hapo.

Akihubiri kwenye Ibada hiyo, Askofu Dk. Malasusa alisema Dayosisi ya Mashariki na Pwani ni pana. Hivyo Washarika wa Usharika huo mpya wana wajibu wa kuanzisha Mitaa na kuitunza.

Katika mahubiri yake alisema kuwa Wakristo wanaokubali kuingia katika Ibada na kumkubali Kristo atawale maisha yao, wanaongezewa rehema, amani na upendo. Na kuongeza kuwa watu wanakaa ndani ya Kanisa, lakini hawajajua thamani ya Kristo.

Aidha aliwaomba Washarika wa Usharika huo, kujituma katika kufanya kazi ya Mungu. Pia kuwataka wasiweke kipaumbele kwenye kulipwa fedha pale wanapofanya kazi katika Kanisa kama vile kupamba au kufanya usafi.

Alisema kuwa Mungu ndiye anayelipa. Katika hatua nyingine Asko fu Malasusa aliwatahadharisha Wakristo kujihadhari na watu wanaotoa mafundisho potofu ya neno la Mungu ambayo yanazidi kuibuka kila siku.

Alisema neno la Mungu limekuwa likiuzwa ama likitolewa kama njia ya kujipatia fedha kwa kuwapotosha watu. Hasa kwa kuambiwa juu ya mafanikio hali ambayo kila mtu anapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari ili asipotoshwe.