MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo amesisitiza kuwa chanjo inayotolewa kwa ajili ya kujikinga na Ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Korona (Uviko 19), haina uhusiano wowote na mpinga Kristo wala alama ya 666 iliyoandikwa kwenye kitabu cha Ufunuo 13.

Askofu Dk. Shoo aliyasema hayo wakati wa kipindi maalumu kilichozungumzia Uviko 19 kilichohusisha viongozi wa dini kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).

Viongozi hao walikutana kutokana na mkakati uliotengenezwa na KKKT, kwa kushirikiana na viongozi hao wengine wa dini na kuunda kikosi kazi maalumu, kilichohusisha viongozi wa dini 13 na wataalamu wawili wa afya kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19. Mkakati wa kikosi kazi hicho ulilenga kuangalia matendo ya kiimani ambayo yanaweza kusababisha maambukizi ya Uviko 19.

Viongozi hao wa dini walizungumzia mambo waliyoyajadili kutoka kwenye kikosi kazi hicho katika kipindi hicho kilichorushwa mubashara na Upendo TV. Hii siyo mara ya kwanza kwa Askofu Dk. Shoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCT, kusema kwamba chanjo hiyo ambayo ilizinduliwa hapa nchini Julai 28, haina uhusiano wowote na chapa ya 666.

Baadhi ya watu walianza kuihusisha chanjo ya Uviko 19 na chapa ya 666 huku wakidai kuwa ndiyo dalili ya mpinga Kristo, kama ilivyoandikwa kwenye Biblia, hususani kitabu cha Ufunuo. Askofu Dk. Shoo alisema kuwa watu wanaouhusisha chanjo hiyo ni Mpinga Kristo ni wale wasiojua maandiko.

“Hao wanaosema hivyo hawaelewi kabisa maandiko matakatifu sawasawa, kwa mtu aliyesoma historia ya Kanisa, historia ya maandiko matakatifu, anaelewa kabisa kuwa hayana uhusiano na mwisho wa dunia wala jambo hilo la Uviko 19,” alisema Askofu Dk. Shoo. Alisema kuwa wanaosema hivyo wana nia ya kuonyesha kuwa chanjo hiyo ina lengo ovu nyuma yake au ni watu wanaotaka kuangamiza Waafrika, kwa hiyo wao wanachokifanya ni kuondoa upotoshaji huo.

Kwa upande wake Askofu Gervas Nyaisonga kutoka TEC, alisema kuwa Kanisa Katoliki limesitisha baadhi ya taratibu za Ibada kama vile kuchovya maji ya baraka, badala yake kwa baadhi ya maeneo wanatumia maji yanayotiririka.

Askofu Nyaisonga alisema kuwa Kanisa Katoliki linaendelea kuwapa elimu waamini wake kuhusu chanjo na kueleza kuwa, Kiongozi wa Kanisa hilo duniani Papa Francis alisema kuwa chanjo ni ishara ya mapendo, kwamba unajipenda na unapenda wengine.

Alieleza kuwa Papa alisisitiza kuwa chanjo hiyo ni muhimu ipatikane kwa wote na iwe imeidhinishwa.

Katibu Mkuu wa BAKWATA, Alhaji Nuhu Mruma alisema kuwa kwa upande wao waliangalia namna ya kuendelea na Ibada katika mazingira ya Uviko huku wakizingatia taratibu zote za Wizara ya Afya.

Mkurugenzi wa Afya wa KKKT, Dk. Paulo Mmbando alisema kuwa chanjo zimekuwa zikitumika kwa muda mwingi kama sehemu ya kuupa mwili askari wa kujilinda dhidi ya magonjwa. “Chanjo zipo za aina nyingi na nyingine zinafanywa mara mbili kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mwili unapata kinga ya kutosha,” alisema Dk. Mruma.

Alitolea mfano wa chanjo ya kifua kikuu na kueleza kuwa watu wengi wanaweza kuishi na wadudu wa kifua kikuu lakini wasipate ugonjwa huo mpaka kitakapotokea kitu cha kushusha kinga yao. “Hili la Uviko ni sehemu ya kawaida kabisa ya chanjo kama zilivyokuwa chanjo za kifaduro, pepopunda na kifua kikuu tofauti yake tu ni kwamba hii ya Uviko inatolewa kwa watu wazima,” alisema Dk. Mruma.

Kwa upande mwingine Askofu Dk. Shoo alisema kuwa, Uviko ni maradhi kama maradhi mengine japokuwa ulipoingia ulisababisha hofu kwa watu kwa sababu ulikuwa ni ugonjwa mpya.

Alisema kuwa Kanisa lilifanya kazi ya kuwaondolea watu hofu. Alisema kuwa Mungu anayo nafasi yake ya kuwaokoa watu wake pale majanga kama hayo yanapotokea, huku akifafanua kuwa wataalamu waliopo ni Mungu ndiye aliyewaweka kwa ajili ya kuwasaidia wanadamu, hivyo hata waliogundua chanjo hiyo ni kipaji kutoka kwa Mungu na wanafanya kazi yao kwa mkono wa Mungu