ASKOFU wa Kanisa la EAGT, Kongwa mkoani Dodoma, Dk. Livingstone Denis amewashauri viongozi wa dini kutotegemea michango na sadaka kutoka kwa waumini na wafadhili, badala yake wajiwekeze kiuchumi ili waweze kuifanya kazi ya Mungu kwa ufanisi mkubwa.

DK. Denis alitoa ushuri huo wakati alipokuwa akitoa taarifa fupi ya hoteli ya kisasa ya Maniyanguru iliyopo Dodoma Makulu, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Athony Mtaka ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa hoteli.

Askofu Dk. Denis ambaye ni mmiliki wa hoteli hiyo alisema kuwa, kitendo cha kutegemea michango na sadaka tu hakiwezi kuifanya kazi ya Mungu kusonga mbele, hivyo ni wakati sasa wa kubuni miradi yenye tija itakayowaletea mafanikio ya kiroho na kimwili. Alisema pamoja na kuifanya kazi ya Mungu, pia wajishughulishe na kufanya kazi kupitia mikono yao, ili waweze pia kuonyesha mfano kwa familia wanazoishi nazo na hata kwa waumini ambao wanaowaongoza kwenye nyumba zao za Ibada.

Alisema kuwa hadi kukamilika kwa hoteli hiyo zimetumika zaidi ya shilingi milioni 500, ambazo zimetokana na juhudi zake katika kuwekeza kwenye kilimo. Kwa upande wake Mtaka aliwashauri viongozi wa dini kutumia fursa zilizopo mkoani Dodoma, kuanzisha miradi itakayowaongezea kipato badala ya kusubiri chombo cha sadaka na ufadhili kutoka kwa marafiki wa nje.

“Niwaombe viongozi wangu wa dini pamoja na waumini, tumieni fursa za uwepo wa Makao Makuu yaliyopo hapa, kwa kuwekeza miradi mbalimbali kama vile kilimo, ufugaji ujenzi wa vitega uchumi kama vile hoteli za kisasa na majengo ya kulala wageni,” alisema.

Aliwataka viongozi hao kuwa mfano kwa waumini wao kwa kufanya kazi kwa bidii, badala ya kuishia kuwahubiria huku wakiendelea kuwa masikini kwenye maisha yao ya kila siku