Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ameongoza ibada kubwa na iliyofana ya kumuweka wakfu na kumsimika Askofu Mteule Geofrey Mwakihaba kuwa Askofu mpya wa KKKT - Dayosisi ya Konde, ibada ambayo imefanyika Kanisa Kuu, Makao Makuu ya Dayosisi hiyo, Rungwe mkoani Mbeya.

 

Tukio la kuingizwa kazini Askofu Mwakihaba limeongozwa na Askofu Mstaafu wa Dayosisi hiyo Dkt. Israel Peter Mwakyolile akishirikiana na maaskofu mbalimbali wa KKKT.

 

Awali kabla ya kumwingiza kazini, Hati mbalimbali zilisomwa na Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo na baadaye Askofu Mstaafu Mwakyolile akatoa maelezo ya kilichotokea na kufanya maombi mazito ya kumwomba Mungu aondoe wakfu kwa Askofu aliyepita, Dkt. Edward Mwaikali.

 

Awali akihubiri katika Ibada ya Siku ya Bwana Kanisania hapo, Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt Shoo amewataka wakristo wakiwemo wachungaji na maaskofu kuwa wanyenyekevu na kumsikiliza Roho Mtakatifu aliye mwezeshaji, kabla hawajachukua hatua yoyote katika maisha yao huku akiwasihi viongozi wapya wa Dayosisi hiyo kuepuka sifa na majigambo yasiyo ya Kimungu na kwamba wakitaka kwenda salama katika utumishi wao wasiwe vifutu.

 

Amewakumbusha kuwa Roho Mtakatifu hapatikani mahakamani wala kwa waganga wa kienyeji wa ndani au nje ya nchi bali ni kwa Mungu pekee.

 

Aidha Askofu Dkt. Shoo ameipongeza na kuipa pole kamati iliyoongozwa na Askofu Dkt. Alex Malasusa huku akieleza kwa undani namna viongozi walivyoumizwa na mgogoro huo na kueleza kuwa mali zote zilizopo mkoa wa Mbeya na Songwe ni mali ya KKKT na si vinginevyo