Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Magharibi Kati (Tabora), Dkt. Isaack Kissiri amesema ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi na haki ya kupata taarifa ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazosababisha ndoa na mimba za utotoni kwa wasichana.

ASKOFU Dkt. Kissiri amezungumza hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuwajengea mazingira wezeshi mabinti-wazazi (teen mothers) na kueleza kwamba, wasichana wengi wamekuwa wakikosa haki zao za elimu ya afya kutokana na tofauti mbalimbali za kijamii na kitamaduni.

Aliongeza kuwa miongoni mwa changamoto nyingine zinazowakabili ni uzazi hatarishi wakati wa kujifungua, jambo ambalo huongeza maradhi na hata ongezeko la vifo vya wajawazito na vichanga vyao.

Askofu Dkt. Kissiri alihimiza kutolewa kwa elimu sahihi, huduma rafiki ya afya ya uzazi na mifumo thabiti ya kuhakikisha vijana wanafikiwa kuanzia ngazi ya familia, taasisi na jamii kwa ujumla.

Alisema kila mwaka takriban wasichana katika umribalehe wanaofikia milioni 16 duniani huzaa na idadi kubwa ya mabinti hao inapatikana katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Aliishukuru Serikali kwa kuruhusu watoto wa kike waliozaa kurudi tena shuleni ili kutimiza ndoto zao, ingawa bado changamoto za kijamii, kitamaduni na kiuchumi zipo na bado zinawakabili.