Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Gehaz Malasusa amesema jitihada za kuendelea kuboresha uchumi wa Wachungaji na Watumishi wengine zinahitajika zaidi kwa kuwa kufanya hivyo kutawasaidia kufanya shughuli za Uinjilisti kwa furaha na nguvu zaidi.

Amesema hayo wakati akizungumza katika hafla ya Shukrani ya Kikundi cha Vikoba cha Muungano wa Wake wa Wachungaji wa Dayosisi hiyo (MUWAWA VICOBA) iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front baada ya Ibada ambapo amewahimiza wake wa Wachungaji ambao hawajajiunga kujiunga haraka ili kuboresha maisha yao.

Askofu Malasusa amewapongeza MUWAWA kwa jitihada na ushirikiano mkubwa walionao hadi kufikia katika mafanikio makubwa na kupewa tuzo ya Kikoba bora Tanzania, amesema kuwa kuna vikundi vingi vimeanzishwa na havikuweza kuendelea kwa muda mrefu na kushindwa kufikia mafanikio, lakini MUWAWA VICOBA wameonyesha mfano wa kuigwa na jamii yote.

Mwenyekiti wa Vikoba hivyo, Anna Mzinga amesema maono ya kuanzisha Vikoba hivyo ni kusaidiana wake wa Wachungaji na Vikoba hivyo havina kikomo na vinaendeshwa Kisasa ikilinganishwa na Vikoba vingine vilivyopo nchini huku akisisitiza umuhimu wa Umoja katika Masuala mbalimbali.

Mlezi wa Kikundi hicho Elika Malasusa amesema tangu kuanzishwa kwa Vikoba hivyo wamefanikiwa Kiuchumi ikiwa ni pamoja na wengi wao kuanzisha biashara ambazo zimewasaidia kupiga hatua kimaendeleo.

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Msaidizi wa Askofu Dean Chediel Lwiza, Wakuu wa Majimbo na baadhi ya Wachungaji kutoka katika Sharika za Dayosisi hiyo.