MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo amekutana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis wakati wa mkutano uliojadili imani na sayansi jijini Vatican.

MKUTANO huo uliokutanisha viongozi wengine wa dini 40, ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF), Mch. Dk. Martin Junge.

Viongozi hao wa dini kutoka pande zote za dunia wamekutana mjini Vatican kujadili athari za mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa 9COP26, ambao unatarajiwa kufanyika Scotland katika mji wa Glasgow, mwishoni mwa Oktoba hadi Novemba 12.

Viongozi hao wametoka katika dini za Kikristo, Waislamu, Wahindu, Wabudha, Methodisti, Uyahudi na nyinginezo.

Juni mwaka huu Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, alikutana na Rais LWF, Askofu Dk. Pant Filibus mjini Vatican katika mkutano wa maandalizi ya miaka 500 ya ungamo la Augsburg, ambayo ni mafundisho yaliyotungwa mwaka 1530 kwa lengo la kuendeleza matengenezo ya Kiprotestanti. Askofu Dk. Shoo ambaye pia ni Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini alitoa hotuba yake mbele ya Papa na viongozi hao 40 kutoka dini mbalimbali duniani na kueleza kuwa, zinahitajika hatua za haraka ili kukomesha mabadiliko ya tabianchi.

“ N i n a a m i n i k w a m b a M u n g u tunayemtumikia na aliyeiumba dunia hii kuwa mahali pazuri kwetu kuishi ni Mungu mwenye neema ambaye kila siku anatupa nafasi na fursa ya kuilinda dunia,” alisema Askofu Dk. Shoo.

Akinukuu kitabu cha Mwanzo 2:25, Mkuu huyo wa Kanisa aliongeza kuwa, jukumu alilopewa Adam na Hawa la kuitunza bustani ya Eden bado lipo hadi leo na kwamba wanadamu wanatakiwa kuitunza dunia dunia ili izae matunda watakayoyafurahia.

“Mabadiliko ya tabia nchi ni tishio kwetu sote, tunalo jukumu la kulinda maisha yetu ya baadaye na wajukuu wetu,” alisema. Askofu huyo alisema kuwa hatua zinatakiwa kuchuliwa sasa bila kuchelewa.

“Kuchukua hatua inamaanisha serikali zetu ziweke hatua kali ambazo zitahimiza matumizi ya teknolojia ya kijani, kutumia maarifa ambayo Mungu amewapa wanasayansi, maarifa ya kupunguza uzalishaji wa kaboni,” alisema

Katika Mkutano huo Dk. Shoo alialikwa kutokana na jitihada zake za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Mkuu huyo wa Kanisa amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kupanda miti hasa katika miteremko ya mlima Kilimanjaro ambao uko katika ramani ya dayosisi anayoiongoza.

Katika Dayosisi anayoingoza ya Kaskazini ni lazima kwa wanafunzi wa Kipaimara kupanda miti na kujifunza juu ya mabadiliko ya tabia nchi. Askofu Dk. Shoo alinukuu maneno ya Martin Luther aliyosema: “Hata kama ningejua kuwa nitakufa kesho, ningepanda mti leo.

” Kwa upande wake Mch. Dk. Junge akizungumza kwa niaba kwa ya jumuiya ya Makanisa ya Kilutheri, alisema watu wenye nia moja kutoka jamii tofauti wanaweza kuungana, kutenda na kufanya kazi pamoja kwa ajili kuhakikisha uzalishaji wa kaboni unapungua na kuwasaidia walio kwenye mazingira magumu.

Katika kuhakikisha kuwa uumbaji unatunzwa, Mch. Dk. Junge alisema LWF imeahaidi kuyapa Makanisa yake rasilimali za kiroho na kitheolojia, ili kuhamasisha hatua za mabadiliko ya tabia nchi na kuzisaidia jamii ambazo zimeathiriwa na mabadiliko hayo.

Akizungumza katika mkutano huo, Papa Francis alisema: “Kila mmoja wetu ana dini yake anayoiamini inayoambatana na tamaduni za kiroho, lakini hakuna utamaduni, siasa au mipaka au vikwazo vya kijamii vinavyotuzuia kusimama pamoja.