Msaidizi wa Askofu wa KKKT - Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Chediel Lwiza amezindua muonekano mpya wa Gazeti la Upendo na kupatikana kwa gazeti hilo mtandaoni ikiwa ni hatua nyingine ya kuliwezesha gazeti hilo kuwafikia watu wengi zaidi duniani kote.

Uzinduzi huo umefanyika kwenye Ibada katika Kanisa la KKKT-DMP, Usharika wa Luguruni na kushuhudiwa na washarika wa usharika huo kwa niaba ya wasomaji wa gazeti hilo.

Akizungumza kwenye Ibada hiyo, Dean Lwiza amepongeza uongozi na watumishi wa Upendo Media kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kuongeza nguvu zaidi katika kazi hiyo ya Mungu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Upendo Media, Theophil Mlaki amewaambia washarika kuwa vyombo vya habari vya Upendo Media ni vya kwao hivyo wanapaswa kuvifuatilia na kuviunga mkono.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upendo Media, Bi Neng'ida Johanes ameeleza kuwa kufanyika kwa uzinduzi huo ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu na kuwashukuru wadau mbalimbali wa vyombo hivyo vya kanisa.