IJUMAA ya Machi 26, 2021 ndiyo siku ambayo mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli ulizikwa kijijini kwao, wilayani Chato mkoani Geita.

Machi 22 mwili wa Hayati Magufuli uliagwa kitaifa mkoani Dodoma ambapo watu mbalimbali walipata fursa ya kuhudhuria msiba huo wakiwamo viongozi wa kiserikali na marais wa nchi mbalimbali, katika tukio hilo kila Rais alipata nafasi ya kuhutubia umma uliojitokeza katika tukio hilo.

Akihutubia umma uliojitokeza siku hiyo, Rais Samia Suluhu alimzungumzia hayati Magufuli akisema, “Alijitolea maisha yake kuwa sadaka kwa Watanzania, hivyo hakuwa na budi kufanya kazi usiku na mchana ili kuwaletea maendeleo Watanzania, sote tulihoji sana kama alipata muda wa kupumzika na familia, hivyo hii ilitusukuma nasi nyuma yake kufanya kazi kwa bidii.” Rais Samia aliendelea kwa kusema;“Kwa tuliofanya naye kazi tunajua saa 24 hazikumtosha, hakuwa na mchana wala usiku, tulizoea kupigiwa simu na kupewa maelekezo muda wowote hata iwe usiku wa manane, bidii yake ilikuwa zaidi ya mchwa, alipenda kuona matokeo na siyo visingizio na lawama.”

Bila shaka hakuna anayeweza kupinga sifa hizo za Magufuli kwa namna ambavyo amekuwa akijituma katika kipindi chake cha uhai wake na katika kipindi cha uongozi wake kama Rais ambapo alikuwa akipambana kuhakikisha nchi inapata maendeleo pia kuhakikisha watu wanaishi kwa usawa.

Moja ya sifa kubwa kwa Hayati Magufuli ni uwajibikaji, katika hili Watanzania wote ni mashuhuda wa namna ambavyo Magufuli alikuwa akiwajibika kwa watu wake hata ule muda ambao alikuwa safarini, wananchi walikuwa wakimsimamisha na kumwambia kero zao.

Alikuwa akisimama kidete kuhakikisha siku hiyohiyo serikali inaanza kutatua kero zilizotajwa na wananchi. Kuna muda ilibidi atumie hata wiki nzima kutembelea na kufanya ziara maeneo mbalimbali ili kuhakikisha miradi iliyo chini ya serikali inafanyika kwa muda husika na kwa wakati husika.

Kuna muda wananchi walikuwa wanamwonea huruma Rais wao kutokana na namna ambavyo alikuwa akiwajibika kwa nguvu kubwa, huku wengi wakijiuliza kama anapata muda wa kupumzika angalau kwa dakika chache.

Sifa nyingine itakayobaki alama kwake ni upendo kwa watu wa hali ya chini, mara kadhaa alikuwa akionesha upendo na namna anavyowajali wanyonge kwa kuwatendea mema ikiwemo kusikiliza shida zao na muda mwingine kuwasaidia watu fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Alama hii ndiyo imefanya watu wengi kujitokeza katika kumuaga kutokana na namna ambavyo alikuwa akiwajali katika kipindi chake cha uongozi.

Ikumbukwe Februari 24 mwaka huu Hayati Magufuli alizindua Kituo cha Mabasi cha Mbezi Luis ambacho kilipewa jina lake na siku hiyo alionesha anavyowajali watu wa hali ya chini kwa kutoa amri ya wamachinga na mamalishe kutobughudhiwa na mtu yeyote katika kituo hicho, kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kuchafua jina lake ambalo kwa heshima kubwa limepewa kituo hicho.

Kwa hayo machache kila mtu anaweza kuona namna hayati, Rais Magufuli alivyokuwa na moyo wa kipekee kutokana na sifa hizo ambazo zinabaki kuwa alama na kumbukumbu ya uongozi wake ambao Watanzania wanaamini utakumbukwa katika vizazi vijavyo.