BENKI inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Maendeleo Bank, imetimiza miaka nane tangu ilipoanzishwa mwaka 2013.

MAENDELEO Bank ilifunguliwa rasmi na aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo Dk. Mohamed Gharib Bilal. Sasa benki hiyo ina matawi manne jijini Dar es Salaam na mawakala karibu kila pembe ya jiji hilo, hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kufikisha huduma kwa wananchi.

Kwa kipindi cha miaka nane imefikia mtaji wa shilingi bilioni 16 kutoka bilioni 4.5 ilioanza nao awali, hii ni hatua kubwa kwa Benki hii ya Kanisa. Ipo mipango mingi iliyoanzisha ya kuwafikia wananchi ambayo imefanywa na Maendeleo Bank, baadhi ikiwa ni kukopesha bodaboda na Bajaj.

Fursa hizi zimechangamkiwa kwa kiasi kikubwa na vijana. Ni dhahiri kuwa Maendeleo Bank imekuwa faraja kubwa kwa watu, na pia mambo inayofanya yanasadifu jina lake la Maendeleo na vijana na wajasiriamali wakiwamo machinga ni mashuhuda wazuri wa hili.

Ni kweli benki inafikia mahali pazuri lakini bado kuna mengi ya kufanya. Ubunifu ambao Maendeleo Bank imekuja nao bila shaka umekuwa na tija kubwa kwa wateja wake, lakini pia unazidi kuwavutia watu wengine kujiunga na benki hiyo.

Kwa mfano baada ya kubuni mipango ya kukopesha bodaboda, bajaji na sasa mpango wa kuwezesha Machinga, bado benki hiyo inaweza kubuni zaidi vitu vingine kama hivyo ambavyo ndiyo mahitaji haswa ya walio wengi katika jamii.

Vijana walliokopa bodaboda na Bajaj wanaweza kuwa mashuhuda, lakini pia wanaweza kupatiwa nafasi ya kutoa shuhuda za namna walivyofanikiwa ili kuwavuta wengine zaidi. Pia wanaweza wakatoa mawazo yao ya namna ya kuboresha zaidi juu ya mikopo hiyo.

Tunaipongeza Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa Maendeleo Bank kwa hatua mliyofikia. Mafanikio yenu yanazidi kuonyesha ni kwa nini Kanisa liliamua kuanzisha benki hii, licha ya ugumu lililokutana nao hapo awali na bado tunatarajia mengi kutoka Maendeleo Bank.