Kanisa la KKKT lachomwa moto

NA PETER MKWAVILA

WATU wasiojulikana wamechoma moto Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Ng’ong’ona, Ushirika wa Ipagala Dayosisi ya Dodoma.

Tukio hilo la ajabu lilitokea hivi karibuni na mbali na kusababisha hasara pia limesababisha waumini wa Mtaa huo kusali nje, huku wakishuhudia magofu ya jengo lao walilolizoea.

Askofu wa Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu alisema kuwa, watu hao walichoma Kanisa hilo na kuteketeza kabisa kila kitu kilichokuwa ndani vikiwamo baadhi ya vifaa vya sakramenti takatifu.

“Tunamwachia Mungu mwenyewe pamoja na kwamba polisi wanashughulika kuwabaini wahusika,” alisema Askofu Kinyunyu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo la kuchomwa Kanisa hilo, alisema taarifa anazo na aliwatuma askari wake eneo la tukio na watakapokamilisha uchunguzi atatoa taarifa sahihi.

UPENDO lilipomtafuta kamanda huyo siku ya Ijumaa Mei 15 alisema kuwa yupo nje ya ofisi.

Askofu Kinyunyu alisema kuwa hakujawahi kuwepo mgogoro dhidi ya Kanisa katika eneo hilo na ndio maana hawawezi kujua chanzo cha kuchomwa moto kwa Kanisa hilo.

Akizungumza na Upendo, Askofu Kinyunyu alisema kuwa Dayosisi imefanya utaratibu wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kujenga Kanisa jingine na michango hiyo itaanza kutolewa Jumapili hii ya Mei 17.

Alisema kuwa Kanisa hilo lilikuwa na uwezo wa kuchukua waumini 100 na uharibifu uliofanyika kutokana na moto huo una thamani ya shilingi milioni 30.

Hata hivyo Askofu alisema kuwa pamoja na kwamba waliofanya hivyo wamewasababishia hasara na kufanya waumini wao kusali nje, Kanisa haliwaombei mabaya, bali linawaombea wabadilike.

“Jumapili iliyopita (Mei 10) sharika zote zilifanya maombi kwa ajili ya janga hilo, tumeombea hilo janga ili Mungu mwenyewe asimame, lakini pia tumemuombea aliyefanya hilo janga atubu, sisi tumemuhesabu huyo ni kama Sauli aliyekuwa anafanya kazi ya kupinga na kuua Wakristo, lakini Yesu alipomtokea alibadilika, hivyo  na sisi tumemuombea abadilike ili aweze kumtumikia Mungu,” alisema Askofu Kinyunyu.

Askofu huyo alisema kuwa, alifika katika Kanisa hilo Jumatatu Mei 11 na kushuhudia washarika wakisomba mchanga kwa ajili ya kuanza kujenga upya Kanisa lao.

“Kwa kweli wana moyo sana na hawajakatishwa tamaa na hayo yaliyowakuta,” alisema.

Mch. Mcharo alisema kuwa kwa sasa Ibada zinafanyika chini ya mti mdogo ulio nje ya Kanisa, lakini kwa sababu ni mdogo wengine wanakaa juani.

Washarika wanalazimika kwenda na viti lakini pia walichukua viti kutoka Usharika wa Ipagala ambao unautunza Mtaa huo ili kukidhi mahitaji.

Alisema kuwa tukio hilo lilikuwa kama msiba kwa Washarika.

Mchungaji huyo alisema kuwa Mtaa huo ulifunguliwa Desemba mwaka jana na bado haujapelekewa Mwinjilisti, ila unapata huduma zote kutoka Usharika wa Ipagala.

Mch. Mcharo alisema kuwa mchungaji msaidizi wa Ipagala ndiye  anaenda kutoa huduma katika Mtaa huo.

 Kwa mujibu wa Mch. Mcharo moto huo uliwashawa Alhamisi ya Mei 7 mwaka huu na Kanisa hilo ambalo lilikuwa limejengwa kwa mbao na mabati liliteketea lote.

Alisema kuwa hapakuwa na mtu Usharikani kwa sababu huduma za kwaya zimesimamishwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa covid 19.

Mch. Mcharo aliliambia Upendo kuwa walitoa taarifa kikosi cha zimamoto lakini hadi wanafika lilikuwa limeteketea.

Waliripoti polisi juu ya tukio hilo na watu wawili walikamatwa lakini mmoja ambaye ni mlinzi wa Mtaa huo aliachiwa kwa dhamana.

Upendo lilizungumza na mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni Katibu wa Mtaa huo,  Emanuel Idabu  ambaye alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea hapakuwa na mtu yeyote ndani.

Idabu alisema kuwa vitu vilivyokuwa ndani ni pamoja viti 90 vya  vya plastiki, meza moja na jenereta moja.

 Alisema walipofika eneo hilo wakati moto unawaka hapakuwa na kiti hata kimoja, jambo ambalo alisema inawezekana wahusika waliiba viti na kuamua kuchoma Kanisa ili kupoteza ushahidi.

“Kwa kweli katika hili hatuwezi kusingizia kuwa ni mgogoro wa kidini, hawa ni watu wenye nia mbaya baada ya kuiba viti wakaona wateketeze Kanisa letu ili kupoteza ushahidi,” alisema