Mwanadamu ana historia ndefu sana katika dunia hii ambayo Mungu ameiumba. Mwanadamu alianguka, Mungu mwenyewe akajichagulia taifa ambalo kwa njia yake angefanya mpango wa wokovu kwa wanadamu wote.

Alianza kwa kumchagua mtu mmoja, Ibrahimu, akamwahidi kwamba angejenga taifa kutoka kwake ambalo lingekuwa mali yake, nalo lingekuwa chombo chake cha kubariki ulimwengu wote.

“BWANA akamwambia Ibrahimu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako. Nawe uwe Baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa wote wa dunia watabarikiwa” Mwanzo 12:1- 3.

Huu ni Unabii wa pili katika Biblia kuhusu kuja kwa Yesu Kristo, ni Baraka ya kiroho inayokuja kwa mtu na kwa Taifa, Baraka za Mungu kwa taifa la Tanzania zinatokana na Injili ya Yesu Kristo kupitia Kanisa lake, kwamba tangu mwanzo kusudi la Kanisa ni kupeleka huduma kwa jamii.

Jamii ipate, elimu, maji safi, chakula, malazi bora, usafiri bora aina zote, nchi kavu, majini, na angani, hospitali, burudani, bidhaabora, ulinzi, pamoja na huduma zote, kimwili, kiakili, na nafsi. Wito wa Ibrahimu haukuwa na ahadi tu, bali majukumu.

Mungu alihitaji kutoka kwa Ibrahimu utii na kujitoa kwake binafsi kama Bwana ili kupokea kilichoahidiwa. Utii na kujitoa vilihitajika, kuliamini Neno lake, kutii maagizo ya Mungu, juhudi za kweli kuishi maisha ya haki, Kanisa siku zote linaomba kwa ajili ya matukio mbalimbali, mwaka huu tutakuwa na kipindi cha uchaguzi, Kanisa lione uadilifu, usawa, kuwajibika kwa kila mtanzania kuhusu taratibu za kisheria tulizojiwekea sisi wenyewe, hakuna jamii isiyokuwa na taratibu hapa duniani, kwa upande mwingine watu wawe na heshima kwa Mungu.

Wafahamu kuwa Mungu ndiye mtawala Mkuu. Ni mkamilifu wa haki. Yeye ni mwenye huruma. Kanisa halitazamii kuona miongoni mwetu wakatokea watu wanaowatia hofu na woga wenzao, uchaguzi upo utapita na ndio maana Mungu ameuruhusu.

Watu wanapaswa kuwa na hofu na Mungu, kuwa na uchaji, kuheshimu wale walio na mamlaka juu yao. “Mwanangu, mche BWANA, na mfalme; Wala usishirikiane na wenye kigeugeu; maana msiba wao utatokea kwa ghafla; Tena ni nani ajuaye uharibifu wa miaka yao” Mithali 24:21-22.

Katika ujirani, watu wenye chuki ndio wale watoao mashtaka ya uongo, ni wale wasioaminika, hasa wakati huu tunapoelekea uchaguzi mkuu, wasemao maneno yasiyofaa. Wenye uchungu mwingi, wanaotaka kuharibu kila kitu.

Kanisa lipeleke habari njema, waionye jamii isikubali jambo lolote ambalo ni baya, watu ambao wanataka kusifiwa, kubembelezwa, wasioweza kujitawala nafsi zao, ni udhaifu mkubwa wa wazi wa tabia zao, Kanisa liiongoze jamii katika hekima ya Mungu, wapuuze watu ambao hawamuogopi Mungu maana watu wa jinsi hiyo hawaaminiki.

Mtu ambaye ana ujuzi kidogo kisha hamuogopi Mungu, na wala haonyeki ni hatari kwa jamii. Watu wazungumzao maneno matamu na mioyoni mwao wanataka kuangamiza ni hatari.

Kanisa linatazamia muendelezo wa kuelewana, mawazo na tabia inayoleta faida kwa Taifa letu, kuaminiana katika kushika nafasi za kuiongoza jamii huleta thawabu kwa Mungu wetu. Tabia ya mtu mara nyingi haijifichi, kile kilichopo moyoni mwake ndicho humtoka, mtu atapimwa kwa matendo na maneno yake, tabia ya mtu ndiyo inayojenga sifa yake.

Mtu mpumbavu harekebishwi kwa kiwango cha hukumu, Serikali kama chombo hakitakiwi kufumbia macho uovu. Watanzania wanataka kuona Mungu anaendelea kuheshimiwa, Kanisa halitegemei kuona serikali isiyo na uthabiti, isiyochukulia hatua waharifu, Kanisa lina uhakika kabisa kuwa watu wanaoishi kwa hofu ya Mungu, wafanyao kazi zao kwa uadilifu, hawana haja ya kuogopa kwa sababu Mungu ana kusudi na taifa hili.

Mtu kamwe asikatae maonyo ya Kanisa kwa sababu ni sauti ya Mungu. Taifa liyapokee maonyo haya ya Kanisa kwa sababu yana makusudi safi, tena ni bora kuliko sauti ya mwanadamu ambayo daima ni ya kujipendekeza, maana wako watu ambao nia yao ni kugandamiza wanyonge, wanachotaka ni kujipatia utajiri kwa njia yeyote ile.

Mungu amewakataa watu wa jinsi hiyo, watu wa jinsi hiyo hudanganya mpaka wazazi wao, hudiriki hata kuwakimbia, huchochea matatizo, huwa na ubinfsi na kudharau maskini na sheria kwa ujumla.

Mungu anasema wazi mtu anayeishi kwa ajili ya ubinafsi wake, siku moja atapata taabu sawa sawa na alivyosababishia watu wengine taabu na mateso. Kanisa linataka kuona hata baada ya uchaguzi Taifa linaendelea kusonga mbele, amani inaendelea kutawala katika jamii, watu wanaishi kama ndugu, wakishiriki kuzitumia rasilimali ambazo kwa upendeleo Mungu ameamua kulipatia taifa hili.

Kamwe asitokee mtu anayedharau neema hii ya Mungu kwa taifa letu, maana kwa umri wa miaka 59, hatukupaswa kuwa hapa tulipo, tulitakiwa tuwe mbali sana, ni ahadi yake Mungu kuwa hataiacha nchi hii tena kuangukia katika kunyonywa, bali sasa wananchi wenyewe kupitia uongozi watakao uweka kupitia nguvu ya Mungu, watasonga mbele, na wengi watatoka mbali na kuja kujifunza kwa watoto wa Mungu walioko katika Kanisa la Tanzania.

Mungu wa milele, Wewe ndiye Muweka ahadi tunayo Imani kubwa kwamba hulali, unaiangalia kwa jicho la pekee nchi hii.Tunakusihi, uisafishe mioyo yetu; watu wako tuendelee kukupa heshima na tukuzo kwa Yesu Kristo.

Amani na iwe kwa nchi ya Tanzania.