•  Ibada za Jumuiya zasimamishwa
  • Mwanafunzi Mtanzania  China azungumza na UPENDO

NA ZACHARIA OSANGA

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limesitisha kwa muda
salamu za kupeana mikono katikati ya Ibada, kwa lengo la kuchukua
tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona ambao umeingia nchini.

Uamuzi huo umetolewa kwenye barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa
Kanisa hilo, Brighton Killewa na kusambazwa kwenda Dayosisi zote 26
za Kanisa hilo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alitangaza Machi 17 mwaka huu, kwamba Tanzania imepata
mgonjwa wa kwanza wa ugonjwa huo, ambaye aligundulika jijini Arusha
akitokea Ubelgiji.

Siku iliyofuata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kufunga shule
zote na mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima
ikiwemo shughuli za michezo, semina, matamasha ya muziki, mikutano
mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali ya shule na
shughuli nyingine za kijamii ambazo si muhimu.

Katika Ibada za KKKT, Washarika hupeana mikono ikiwa ni salamu ya
kutakiana amani kama inavyoelekezwa kwenye liturgia ya Kanisa hilo la
pili kwa ukubwa hapa nchini.

Salamu hiyo huwa sehemu ya tatu ya Ibada ambayo huambatanisha salamu,
somo, imani na mahubiri.

Kiongozi wa Ibada (kwa kufuata kitabu cha Tumwabudu Mungu Wetu) hutoa
ruhusa ya kila mmoja kuwageukia jirani zake walio kulia, kushoto,
mbele na nyuma yake na kupeana mikono na kusema ‘amani ya Bwana iwe
nawe.’

Badala yake sasa watakuwa wanaimba wimbo namba 325 ‘Mahali ni
pazuri.’

DMP YASIMAMISHA IBADA ZA JUMUIYA

Dayosisi ya Mashariki imeendelea kuchukua hatua za tahadhari kwa
ugonjwa huo kwa kusimamisha mikusanyiko ya katikati ya juma kama
vile, Ibada za nyumba kwa nyumba (Jumuiya), mazoezi ya kwaya, semina,
warsha na Ibada nyingine za katikati ya juma isipokuwa Ibada ya
Jumapili na Jumatano ya Majivu.

DMP imeelekeza milango ya Ibada iwe wazi kwa maombi binafsi.

WAKUU WA SHULE WAKIRI ATHARI

Kutokana na serikali kufunga shule na vyuo, baadhi ya wakuu wa shule
za Kanisa walizungumzia sakata hilo na kukiri kuwa janga la corona
limewapa athari.

Mkuu wa Shule ya Seminari Ndogo ya Kisarawe, Ntekaniwa Godfrey,
inayomilikiwa na Dayosisi ya Mashariki na Pwani, aliliambia UPENDO
kuwa  wametekeleza agizo la serikali la kufunga shule na kusema kuwa
wanafunzi wote wameshaondoka kwenda makwao.

“Baada ya tangazo kutoka, tuliwapigia wazazi na kuwaeleza juu ya
agizo la serikali, wakati huo hatukuwa bado tumewaambia watoto,
tunashukuru Mungu wazazi walifanya haraka kuja kuchukua watoto na
wengine kutuma nauli,” alisema Mwl. Ntekaniwa.

Mkuu huyo wa shule alisema kuwa wanafunzi hao waliondoka kesho yake
na kwa sasa hakuna mwanafunzi yeyote shuleni hapo.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Lwandai ya Dayosisi ya Kaskazini
Mashariki (Tanga), Mch. Happiness Shoo alisema kuwa wanafunzi katika
shule hiyo walifanikiwa kuondoka lakini akasema kuwa wataingia
gharama kwa sababu vyakula walivyokuwa wamenunua vitaharibika.

“Vyakula vile ambavyo vinaweza kuhifadhika vitakuwa salama lakini kwa
hivi vingine ni hasara,” alisema mkuu huyo wa shule na kuongeza kuwa
pia wanashukuru wazazi waliitikia kwa haraka kwenda kuwachukua watoto
wao baada ya kuwapa taarifa za kufunga shule.

Mkuu wa Shule ya Wasichana Mkuza ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani,
iliyopo mkoani Pwani, Grace Mmbaga alisema kuwa walipotoa taarifa kwa
wazazi juu ya kufunga shule, wazazi walifika kuwachukua watoto wao
lakini pia akaongeza kuwa programu za shule zimeathirika kwa sababu
walikuwa wanajiandaa kwa mitihani na kwamba pia walikuwa wamepanga
kumaliza mtaala kwa muda waliokuwa wamejiwekea jambo ambalo
halitawezekana kwa sasa.

Mch. Mmbaga alisema pia vyakula walivyokuwa wameviweka vitaharibika
na wanaangalia utaratibu gani waufanye ili kuvinusuru.

Alisema ili kulinda uwezo wa wanafunzi hao wamewaandalia kazi ambazo
watakuwa wanazifanya kipindi hiki cha likizo ya dharura.

Mkuu wa shule ya Nronga ya Dayosisi ya Kaskazini, Esther Nkya alisema
kuwa baada ya tangazo hilo, siku iliyofuata  wanafunzi wote
waliondoka isipokuwa wale waliokuwa wanatoka mikoa ya mbali (Mwanza),
ambao waliondoka Aprili 19.

Mwl. Nkya alisema kuwa mitaala haitaenda sawa kutokana na hali hiyo
ya dharura na ratiba nyingine za walimu hazitaweza kuendelea.

MAKANISA YAFUNGWA

Ugonjwa corona umeleta baa jipya ambalo labda halijawahi kutokea.
Baadhi ya makanisa katika baadhi ya nchi yamesimamisha Ibada hadi
pale hali itakapotengemaa.

Dayosisi ya London ya Kanisa la Anglikana imesimamisha Ibada zote
mpaka mwezi Mei ili kujikinga na ugonjwa huo ambao umeua maelfu ya
watu.

Aidha, Ibada za mazishi pia zimezuiliwa badala yake ndugu wa karibu
tu ndiyo wanaruhusiwa kuuzika mwili wa mpendwa wao na kufanya Ibada
ya mazishi makaburini.

Vilevile Ibada za ndoa na Kipaimara nazo zimesogezwa mbele sawia na
Ibada za Ubatizo.

Huko nchini Marekani katika mji wa Atlanta, makanisa yamepanga
kuendesha Ibada kwa njia ya mtandao badala kukusanyika pamoja.

Nchini Kenya, gazeti la Daily Nation liliripoti kuwa, Kanisa
Presbyterian la Afrika Mashariki (PCEA) na Kanisa Kuu la Watakatifu
wote la jijini Nairobi, nayo yamefunga utaratibu wa Ibada za Jumapili
kwa muda wa majuma matatu, lakini milango ya makanisa hayo itakuwa
wazi kwa kipindi hicho kwa ajili ya maombi binafsi.

Hata hivyo, PCEA iliwatangazia waumini wake takribani milioni 4.5
kuendelea kuomba na kwamba litaendesha Ibada kwa njia ya mtandao.

IBADA YA NDOA WATU WATANO TU

Kanisa hilo pia lilisema kuwa Ibada za ndoa zitafungwa kukiwa na watu
watano ambao Bwana na Bibi Harusi, wadhamini wawili na Mchungaji.

KUNAWA MIKONO

Makanisa hapa jijini Dar es Salaam yamezingatia maagizo ya Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na  Watoto kwa kunawa mikono
kabla na baada ya kutoka kwenye nyumba za Ibada.

Sabuni maalumu zimewekwa kwenye milango na washarika wamekuwa makini
katika kuzingatia hilo pamoja na kuepuka kusalimiana kwa kushikana
mikono.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mtu anatakiwa kunawa mikono kwa
sabuni au maji yanayotiririka ili kuua bakteria wanaosababisha
COVID-19.

Pia inatakiwa kuepuka kushikana mikono kwa sababu virusi vya ugonjwa
huo vinaweza kubaki kwenye viganja na kumwambukiza mtu mwingine kwa
urahisi.

Virusi hivyo pia vinaweza kubaki kwenye viganja vya mikono endapo
mwathirika atapiga chafya na kujizuia kwa mikono yake. Inaelezwa kuwa
endapo mtu atapiga chafya virusi hivyo vinaweza kuruka kwa umbali wa
mita moja, ndiyo sababu watu wanashauriwa kuvaa barokoa (mask) na pia
kutosogeleana sana.

MZOZO CHINA NA MAREKANI

Hivi karibuni China iliishutumu Marekani kwamba ndiyo iliyopeleka
kirusi hicho cha corona katika mji wa Wuhan mwishoni mwa mwaka 2019.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya China alidai kuwa Marekani ilipeleka
kirusi hicho kwa kutumia jeshi.

Rais Donald Trump wa Marekani alikoleza zaidi mzozo huo wa chinichini
pale alipoandika kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba corona ni
kirusi cha Kichina.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, Wachina walikerwa na kauli
hiyo ya Trump na kumtaka aache kauli hizo za kibaguzi na kuinyanyapaa
China.

Hata hivyo, gazeti NewYork Times lilimnukuu Rais Trump akisisitiza
kuwa kauli yake siyo ya kibaguzi kwa sababu ni kweli kwamba virusi
hivyo vinatoka China.

MWANAFUNZI   WA TANZANIA CHINA AZUNGUMZA

Martin Kawamala ni mwanafunzi wa Kitanzania anayesoma Chuo Kikuu cha
Geosciences (GUG), alizungumza na UPENDO kutoka mji wa Wuhan
ulipoanzia ugonjwa huo na kusema kuwa baadhi ya shughuli zimeanza
kurudi kama kawaida, lakini bado hawajaruhusiwa kutoka.

Leo (Ijumaa) ni siku ya pili hakuna maambukizi mapya, bado
hatujaruhusiwa kutoka nje nadhani  wanaendelea kujiridhisha,
nilisikia kuwa tunaweza kuwekwa ndani kwa siku 14 ili wajiridhishe
kuwa hamna maambukizi,” alisema Kawamala ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Wanafunzi Watanzania wanaosoma katika Chuo Kikuu hicho cha
Geosciences.

 Kawamala alisema kuwa huko ndani walipo wanaonana kidogo japo
haijawa rasmi lakini wanatembeleana.

 Akizungumzia hali ilivyokuwa wakati walipozuiwa kutoka nje, Kawamala
alisema kuwa, hakuna aliyekuwa anaruhusiwa kusafiri kwenda sehemu
nyingine na baadaye walienda mbali zaidi na kuzuia hata kutoka nje ya
hosteli.

“Mwanzon tulikuwa tukiruhusiwa kwenda supermarket, baadaye wakaja
kuzuia kutoka nje, ila walikuwa wakijitahidi kuwaletea chakula
wanafunzi na pia kukawa na huduma za kununua chakula mtandaoni,  hii
ni kwa mujibu wa chuo chetu tu lakini kwingine pia kulikuwa na
changamoto zao tofauti na hapa,” alisema.

MAELFU WAFA

Hadi Machi 19 jumla ya watu 9,829 walikuwa wamefariki kutokana na
ugonjwa huo ambao ulianzia katika mji wa Wuhan, China mwishoni mwa
mwaka 2019 na watu 236,920 wakiwa wameambukizwa.

Italia inaongoza kwa vifo vingi ikiwa imeipita China, watu 3,405
wamekufa nchini humo wakati China ambayo maambukizi yamepungua ikiwa
na vifo 3,245.

This news is from UPENDO, the weekly newspaper of ELCT Estern and
Coastal Diocese.
Follow us on Facebook , Instagram and Youtube.