Malasusa azindua jengo la watoto Kijitonyama

NA VICENT KASAMBALA

ASKOFU wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dk. Alex Malasusa, amezindua jengo la Ibada ya watoto wa shule ya Jumapili Usharika wa Kijitonyama ambalo litagharimu shilingi milioni 916.6 pale litakapokamilika kabisa kwa kuwekewa lifti na samani.

Akizindua jengo hilo Askofu Malasusa aliwapongeza washarika wa Kijitonyama kwa kazi waliyofanya kwa ajili ya watoto wao na kusema kuwa, watoto wengi hasa wa kizazi hiki hawaijui vizuri imani yao kutokana na kukosa misingi mizuri ya mafundisho wanayotakiwa kuyapata.

Alisema wazazi lazima wawafundishe watoto wao misingi ya imani na maadili tangu wakiwa wadogo kwa sababu kwa kufanya hivyo watakuwa wanaendeleza imani kwa vitendo na watakuwa baraka kwa familia, jamii, kanisa na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Askofu Malasusa alisisitiza umuhimu watoto wote wanaotaka kupata Kipaimara kuhakikisha wanazingatia kwanza mafundisho, huku akiwataka wazazi kuacha kuwasumbua Wachungaji ili watoto wao wapate Kipaimara bila mafundisho kutokana na sababu mbalimbali.

Mmoja wa Watoto wa Usharika huo, Ivo Kombo akisoma risala kabla ya ufunguzi huo,  alisema kupitia jengo hilo watoto wanajisikia wenye thamani kubwa ndani ya Kanisa, huku akiendelea kuwaomba wazazi na viongozi wa Kanisa kuendelea kuwajali na kuwapenda.

Watoto hao waliwashukuru wabeba maono wa kazi hiyo, Mch. Eliona Kimaro pamoja na Baraza la Wazee likiongozwa na Katibu wa Baraza, Dk. Victoria Kisyombe na wajumbe wa kamati ya ujenzi wa jengo wakiongozwa na Mwenyekiti Dk. Hans Macha kwa kuona watoto wanapaswa kuwa na jengo zuri lenye madarasa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya ibada.

This news is from UPENDO, the weekly newspaper of ELCT Estern and Coastal Diocese.
Follow us on Facebook , Instagram and Youtube.