
WAKATI Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) likitarajiwa kutimiza umri wa miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, imebainika kuwa Kanisa hilo la pili kwa ukubwa nchini, linamiliki na kuendesha mamia ya taasisi za huduma za jamii, huku likifanya matendo ya huruma kwa wahitaji.
WAHITAJI hao wamekuwa wakipata huduma kupitia makumi ya vituo vya diakonia. Udiakonia kwa mujibu wa Katiba ya KKKT, toleo la mwaka 2015 ni huduma ya upendo na huruma. Pia, KKKT linamiliki taasisi nyingine ambazo hutoa huduma za kijamii. Taasisi hizo ni pamoja na zile za elimu 120, afya 172 zikiwamo hospitali 24.
Katika Mkutano Mkuu wa Kanisa hilo uliofanyika mwaka 2019 katika Dayosisi ya Kaskazini Kati (Arusha), Mkuu wa Kanisa hilo, Ask. Dkt. Fredrick Shoo, alisema KKKT inachangia asilimia 24 ya huduma za afya kote nchini. KKKT litafikisha miaka 60 ifikapo Juni 19, 2023 na tayari Mkuu wa Kanisa Askofu Dkt. Shoo ametoa wito kwa Dayosisi na washarika wote kushiriki maadhimisho hayo katika ngazi mbalimbali za Kanisa.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Diakonia wa KKKT, Dkt. Paul Mmbando anasema huduma za jamii zimewagusa wengi bila kujali dini wala madhehebu yao. Taasisi za elimu, afya na udiakonia za KKKT zipo chini ya umiliki wa Dayosisi za Kanisa hilo ambazo ni 27, lakini zipo zinazomilikiwa kwa umoja chini ya Kanisa. Hizo ni kama Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira kilichopo mkoani Arusha na Shule ya Seminari Ndogo ya Morogoro (Lutheran Joniour Seminary).
Kwa mujibu wa Dk. Mmbando Shule za sekondari zilizopo chini ya KKKT ni 67, shule za msingi 17, vyuo vya ufundi 21 vyuo vikuu na vikuu vishiriki 6. “Huduma hizi zimewagusa watu wengi wanaoishi vijijini, kwani taasisi nyingi za dini ziko huko na watu wengi wanaoishi huko wana mzigo mkubwa wa kiuchumi kwani wanategemea kilimo na ufugaji,” alisema Dkt. Mmbando.
Pamoja na kwamba wito mkuu ni kumhudumia mtu kiroho, KKKT pia inatoa kipaumbele kwa huduma za udiakonia kwa lengo la kumhudumia binadamu kiakili na kimwili na hii ndiyo sababu ya kuwa vituo hivyo vya elimu, afya na diakonia. Dkt. Mmbando alivitaja vituo vya huduma za udiakonia kuwa ni kituo cha Mwanga mkoani Kilimanjaro cha shule ya viziwi Mwanga.
Kwa upande wa Dayosisi ya Kaskazini (Moshi – Kilimanjaro) ni Faraja na Hai ambavyo vinaangalia watoto wenye ulemavu wa viungo. Katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk. Mmbando anasema kuna kituo cha Irente kinachohudumia watoto wasioona na viziwi, wakati Dayosisi ya Mbulu ina kituo cha Dongobesh kinacholea watoto viziwi. Nyingine ni Dayosisi ya Mashariki na Pwani (Dar es Salaam) ambayo inaendesha kituo cha Mtoni ambacho kinalea watoto wenye ulemavu wa akili.
Hivi sasa Dayosi hiyo inajenga Chuo cha Ufundi Mlandizi kwa ajili ya kuwahudumia watoto hao baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Kwa upande wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi (Bukoba – Kagera) Dk. Mmbando anasema kipo kituo cha Watoto yatima Ntoma, Senta ya Watoto Tumaini, Kituo cha wasiojiweza Igabiro na Shule ya Diakonia Ntoma.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa Udiakonia ndani ya KKKT ni kwa ajili ya maendeleo ya watu kwa manufaa ya watu, hasa wenye kipato cha chini au wagonjwa, maskini, watoto yatima, wajane na watu wasiojiweza. Alifafanua kwamba katika Udiakonia hufanyika mambo mengi mbali na elimu na afya, ikiwemo utunzaji wa mazingira (uumbaji wa Mungu) ambao hujumuisha upandaji wa miti.
Kuhusu suala la afya, Dk. Mmbando anasema watu wenye magonjwa makubwa kama vile saratani wanaweza kuchelewa kufika katika huduma husika, hivyo Kanisa linapopeleka huduma hizo linalenga watu ambao wana uhitaji bila kujali, uchumi wao, kabila au dini. Anaeleza kuwa lengo la Kanisa ni kuwashika watu mkono wanapokuwa wameanguka na kukutana na changamoto mbalimbali, huku akilitaja eneo jingine ambalo Kanisa linaliwekea mkazo kuwa ni watu kupata lishe, elimu, chakula na huduma bora ya afya.
Dk. Mmbando anasisitiza kuwa Kanisa pia linaangalia suala zima la amani kwani kazi ya dini ni kuwatuliza watu, kuepusha migogoro ili amani izidi kutawala. Huduma za jamii katika Dayosisi
DAYOSISI YA KASKAZINI (MOSHI NA KARATU)
Dayosisi ya Kaskazini ina shule za sekondari 12 na shule za msingi nne. Kwa upande wa Vituo vya Afya kuna Taasisi ya Mafunzo ya Afya Machame na Taasisi ya Mafunzo ya Afya Karatu (Arusha). Dayosisi hiyo pia inamiliki Hospitali za Marangu (Kitemboni), Machame na Hospitali Karatu. Pia inamiliki Chuo cha Mafunzo ya Montessori - Usharika wa Neema, Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi na vyuo vingine vya mafunzo ya ufundi vinne. Hali kadhalika ina vituo vingine vya udiakonia ambavyo ni Usharika wa Neema Convert, Kalali Orphanage and Helen Memorial Centre na Shule ya Msingi Maalumu Faraja.
DAYOSISI YA KASKAZINI MAGHARIBI (BUKOBA- KAGERA)
Dayosisi hii naendesha Shule za Sekondari tatu, Shule za Msingi tatu na Vyuo vya Ufundi Stadi Ntoma na Muleba. Kwa upande wa Hospitali na vyuo vya Uuguzi, inaendesha Hospitali za Ndolage na Izimbya, Chuo cha Uuguzi na Ukunga Ndolage, Chuo cha Maofisa Tabibu Ndolage, Kituo cha Afya cha KKKT Bukoba Mjini na kituo cha afya cha Rwantege. Ina jumla ya zahanati tisa. Pia wana Mradi wa kuelimisha Yatima Missenyi (MOSS), Kituo cha useremala cha Olemera kwa Watoto yatima (ICCO), Kituo cha Ufundi Stadi Huyawa-A, na wanaendesha Programu ya Huduma ya Watoto (HUYAWA), Programu ya Shauku na huduma ya mtoto na huruma na Makao makuu ya Masista Namalira. Dayosisi hiyo pia ina vituo vya diakonia kama ilivyoelezwa na Dkt. Paul Mmbando ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Diakonia wa KKKT mwanzoni mwa habari hii.
DAYOSISI YA KARAGWE (KAGERA)
Kwa huduma za Afya Dayosisi wana hospitali moja na ya Zahanati nne. Pia wana mradi wa utetezi wa Watoto wanawake na Albino wa Kanda (ShauKU), Mradi wa Age (Adolescent Girls Empowerment), Mradi wa GCE (Girls Child Empowerment. Kwa upande wa elimu wanazo shule za Sekondari tatu, shule tatu za msingi, shule tatu za Kiingereza na Chuo Kikuu cha Karagwe (KARUCO). Dayosisi hiyo pia ina Chuo cha Ufundi na Maarifa ya Nyumbani Nkwenda, Shule ya ufundi ya watoto yatima Lukangaje na Chuo cha Ufundi EMAU Nyaishozi.
DAYOSISI YA KUSINI
Dayosisi ya Kusini iliyopo mkoani Njombe, ina shule za sekondari sita, shule moja ya awali na msingi na Kituo cha Elimu Emmaberg. Pia ina kituo cha Mafunzo ya ufundi stadi cha Kilutheri Mafinga na Usimamizi wa Chuo cha Amani na Teknolojia (ACMT). Pia inamiliki vituo vya huduma kwa jamii vya Ilembula Institute of Health and Allied Sience (IIHAS), Ilembula Lutheran Hospital (ILH) na Kituo cha Afya Kidugala. Wanavyo vituo vya malezi ya watoto yatima Mafinga na Ilembula, Kituo cha Wazee Usharika wa Kibena, Waseja Faraja Centre na Kituo cha mafunzo ya ufundi cha Kilutheri, Ilembula.
DAYOSISI YA MASHARIKI NA PWANI (DAR ES SALAAM)
Dayosisi hii ina Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco) na Chuo cha Elimu Maneromango. Inazo Shule za Sekondari tatu, shule ya awali na msingi moja. Pia ina Kituo cha afya cha Mtoni na zahanati nyingine tatu. Visiwani Zanzibar, DMP inaendesha kituo cha Upendo Women Empowerment Ltd na Zanzibar Interfaith Centre (ZANZIC).
DAYOSISI YA KASKAZINI MASHARIKI (LUSHOTO - TANGA)
Dayosisi hii ina Hospitali Teule ya Kilindi, Hospitali ya wagonjwa wa akili (Lutindi Mental Hospital) na Outreach. Pia ina Shule za Sekondari mbili, Msingi tatu na chuo kimoja cha Koketi.
DAYOSISI YA KATI (SINGIDA)
Dayosisi hiyo ina Hospitali ya Kilutheri ya Iambi, zahanati 10 na Chuo cha Uuguzi kimoja cha Iambi. Pia ina Shule za Sekondari tatu.
DAYOSISI YA MBULU (MANYARA)
Inavyo vituo vya afya vitatu, Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi za Afya Haydom na Hospitali ya Rufaa ya Kilutheri Haydom.Dayosisi hii ina Shule moja ya Sekondari. DAYOSISI YA PARE (KILIMANJARO) Inamiliki Shule za Sekondari mbili na Hospitali moja ya Gonja Lutheran.
DAYOSISI YA KUSINI KATI Dayosisi hiyo ina Chuo cha Semina na Mafunzo Madihani na Kituo cha Tumaini Kidope kilichopo Bulongwa. Pia wanacho kituo cha Udiakonia Tandala na kwa upande wa afya wanayo Taasisi ya Sayansi za Afya (BHSI) na Hospitali ya Lutheran Bulongwa na zahanati sita. Pia wanayo shule ya sekondari Bulongwa.
DAYOSISI YA KONDE (MBEYA)
Dayosisi hii ina hospitali mbili, kituo cha kulea watoto cha Iwambi na kituo cha Mafunzo Mwakaleli. Pia wana chuo cha ufundi stadi Matema na Shule ya Seminari ndogo ya Kilutheri Manow.
DAYOSISI YA KASKAZINI KATI (ARUSHA)
Dayosisi hii ina shule za sekondari ni sita, shule za msingi tatu na Chuo cha Ufundi Olokii. Kwa upande wa afya, inacho Kituo cha Arusha Lutheran Medical Centre, Hospitali ya Kilutheri Selian, Hospitali ya KKKT Orkesemet na kituo cha afya Kirurumo-Mto wa Mbu. Vituo vingine ni kituo cha mafunzo cha ALM (ALMMT-TC)
DAYOSISI YA IRINGA
Dayosisi hii ina Hospitali ya Ilula, zahanati tisa, Chuo cha Uuguzi Ilula na Chuo Kikuu cha Iringa. Pia ina kituo cha Huruma (Kituo cha Watoto yatima na mazingira magumu). Kwa upande wa elimu inazo shule za sekondari sita na shule za awali tatu.
DAYOSISI YA DODOMA
Dayosisi hii ina Shule za Sekondari mbili na zahanati mbili. Pia ina kituo cha ufundi cha KKKT Hekima, City College of Allied Sciences Dodoma na Hekima Hope-Hamai Vocational Training Centre (Chuo cha ufundi hekima Tawi la Kondoa) na kituo cha mafunzo ya ufundi cha Hekima CUPU.
DAYOSISI YA MASHARIKI YA ZIWA
Dayosisi hii ina zahanati moja ya Imani. Shule za Sekondari ni moja na wana kituo cha Ushauri wa Kisaikolojia.
DAYOSISI YA MKOANI MARA (MUSOMA)
Dayosisi hii ina Hospitali Teule ya Bunda na Zahanati ya KKKT, Tarime. Upande wa elimu wana shule ya Sekondari ya Ufundi Samaritani, Shule ya Msingi Sirari, Shule ya Sirari Samaritan English Medium na Shule ya Kilutheri ya Angaza.
Vituo vingine ni Kituo cha huduma ya mtoto Tarime, kituo cha huduma ya mtoto Mwisege na kituo cha huduma ya mama na mtoto Bunda.
DAYOSISI YA MERU (ARUSHA)
Dayosisi ina kituo cha watu wenye ulemavu Usa-River, Shule za Sekondari tano, Chuo cha ufundi stadi cha Lugeruki pamoja na Kituo cha elimu Leguruki/King’ori. Kadhalika wana kituo cha mafunzo ya ufundi Mshikamano (Mshikamano Vocational Training Centre). Upande wa afya wanayo Hospitali ya Kilutheri ya Nkoaranga, Kituo cha afya Lugeruki na zahanati mbili. Pia wanaendesha kituo cha watoto yatima.
DAYOSISI YA KUSINI MAGHARIBI (MATAMBA)
Dayosisi hii ina shule ya sekondari moja ya Itamba, Kituo cha afya Magoye na Zahanati tatu huku ikiwa na shule za awali tatu.
DAYOSISI YA ULANGA KILOMBERO (MO- ROGORO)
Dayosisi ina Hospitali ya Kilutheri Lugala, zahanati mbili na Chuo cha Uuguzi Lugala. Wanamiliki Shule moja ya sekondari, shule za awali saba na Seminari ya Kilutheri Tumaini. Pia wana kituo cha huduma ya mtoto Kanisa Kuu Milola na Kituo cha huduma ya mtoto Mbingu.
DAYOSISI YA MOROGORO
Dayosisi hii ina Zahanati ya Mkulazi, Kituo cha Wanawake Kimbilio pamoja na Kituo cha Women Power. Pia wana shule moja.
DAYOSISI YA KUSINI MASHARIKI YA ZIWA VOCTORIA (SIMIYU)
Dayosisi ina shule moja ya sekondari, shule za msingi tatu, kituo cha mafunzo cha Bishop Emmanuel Makala na huku wakiwa na zahanati mbili. Pia wanacho kituo cha watoto yatima Bariadi pamoja na kituo cha kulea watoto wenye Ualbino na watoto wenye mazingira magumu.
DAYOSISI YA KUSINI MASHARIKI (LINDI NA MTWARA)
Wanayo shule ya sekondari moja na shule nne za chekechea. Pia wanacho kituo cha Compassion -Magomeni Lutheran.
DAYOSISI YA RUVUMA (SONGEA)
Dayosisi ina kituo cha watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi cha Jirani mwema, Shule ya msingi moja na Shule ya Sekondari moja. Pia wana Shule ya Bishop Amon Mwenda Kindergaten Centre, na shule ya chekechea Tumaini.
DAYOSISI YA ZIWA TANGANYIKA (RUKWA NA KATAVI)
Katika Dayosisi hii kuna kituo kimoja cha Afya Mtisi.
DAYOSISI YA MWANGA (KILIMANJARO)
Dayosisi ina shule ya sekondari moja, kituo cha Afya Shighatini na kituo cha Mafunzo na Uongozi, Usangi.