Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, inajiandaa kufanya Mkutano Mkuu wake wa 36 ambao utafanyika kwa siku nne kuanzia Jumapili ya Novemba 27 hadi 30, 2022 katika Usharika wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Mkutano Mkuu wa Dayosisi hufanyika kila baada ya miaka miwili na ndiyo chombo kikuu cha maamuzi ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Baadhi ya mambo ambayo tunayapa kipaumbele katika mkutano huu ni pamoja na kujadili utekelezaji wa kazi mbalimbali zilizofanyika katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kupanga mipango mingine ya miaka miwili ijayo kulingana na Mpango mkakati wa Dayosisi. Mkutano pia utajadili maendeleo ya Dayosisi katika nyanja ya kuhubiri Injili na huduma za jamii ikiwemo huduma afya, elimu, makundi maalum na mwenendo wa hali ya kiuchumi kwa ujumla.

Mkutano Mkuu utaongozwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt ALEX GEHAZ MALASUSA ukiwa na wajumbe 424 ambao kati ya hao ni Wachungaji wote wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani. Wajumbe wengine ni pamoja na wawakilishi wa mabaraza ya wazee kutoka sharika 97 na mitaa 208 na wawakilishi kutoka Majimbo sita ya Dayosisi yetu, Vituo vikiwemo Maendeleo Bank, Upendo Media, Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, (TUDARCO) na taasisi zake nyingine.

Katika Mkutano huo pia kutakuwa na uchanguzi wa Wenyeviti wa Halmashauri za Idara na Bodi za Vituo.

Neno Kuu la Mkutano wa mwaka huu linasema: “Bwana Mmoja, Imani mmoja, Ubatizo mmoja” Waefeso 4: 5.