Waumini wa Kikristo wamekumbushwa kuwa na tabia ya utii na unyenyekevu na kuwaheshimu watu wote, kwa sababu hizo ndizo tabia alizokuwa nazo Bwana Yesu wakati akitumikia wito wake hapa duniani.

Akihubiri katika Ibada iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilitheri Tanzania, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika Mteule wa Mongolandege, Mwinjilisti wa Usharika huo Mteule Edward Maarifa alisema kuwa Wakristo wanatakiwa kufuata mwenendo wa Bwana Yesu Kristo ambaye aliwapenda watu wote wakiwamo wanyonge na waliodharauliwa.

Mwinjilisti Maarifa alisema kuwa, Yesu hakubagua mtu yoyote na ndiyo sababu hata wanafunzi wake walipojaribu kuwazuia watoto wadogo wasimsogolee yeye aliwakataza na kuwapa nafasi watoto ambayo walikuwa wakizuiwa, lakini zaidi hayo alisema kuwa Yesu anapenda watu wote na kwamba mtu anayewajali wanyonge atapendwa na watu.

Akifafanua juu ya Yesu kupanda punda huku watu wakimtandikia nguo zao na mitende, alisema kuwa mtu yeyote anapokuwa ana Yesu anaheshimiwa kama ambavyo punda alipata heshima ya kutembea juu ya nguo za watu, lakini bila kuwa na Yesu hakuna heshima hiyo.

Mwinjilisti Maarifa alisema kuwa, mtu ambaye amempokea Yesu moyoni anajijengea heshima kwenye jamii kama vile Yesu alivyopewa heshima na watu waliompokea Yesu akiwa amepanda Punda, wakati akiingia Yerusalemu huku wakiwa wameshika matawi ya mitende.

“Katika hali ya kawaida siyo rahisi kwa watu kumuacha punda akanyage nguo zetu, lakini kwa sababu alikuwa amembeba Yesu aliwekewa nguo azikanyage. “Siku ile punda alishangalia lakini siku nyingine aliporudi katika njia ileile alinyanyapaliwa, kwa nini? Kwa sababu hakuwa na Yesu, kama huna Yesu unakosa heshima,” alisema Mwinjilisti Maarifa.

Katika Ibada hiyo washarika waliingia Ibadani kwa maandamano huku wakiwa wameshika matawi ya mitende. Wakati huohuo, Mwinjilisti Maarifa alitoa wito kwa Washarika na watu wote wenye mapenzi mema na kazi ya Mungu, kuendelea kujitoa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Ibada la Usharika huo linaloendelea kujengwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, Christina Mwingira, baada ya Ibada Usharikani hapo, Mwinjilisti Maarifa alisema kuwa wanajiandaa kuanza kufanya Ibada kwenye jengo hilo japo halijakamalika ili kuhamasisha kasi ya ujenzi wa jengo hilo.

Alisema kuwa wanatarajia kwenye Krismasi ya mwaka huu, watasalia katika jengo hilo ingawa bado halijakamilika.