Wapendwa washarika wote wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), nitumie nafasi hii kuwapa salaam za upendo kutoka katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Kanisa lenu, unaoendelea hapa Jijini Arusha.

Viongozi wakuu wa Dayosisi zote, ikiwa ni pamoja na Maaskofu, Makatibu wakuu, pamoja na wajumbe wengine katika umoja wao wanatuma salaam nyingi kwenu.

Pamoja na kwamba katika kikao hiki zinajadiliwa kazi za Kanisa katika wajibu wake wa kufanya missioni ya Mungu hapa duniani, mkutano huu wa Halmashauri Kuu umepata nafasi ya kupokea taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa kushughulikia mgogoro wa KKKT Dayosisi ya Konde.

Wapendwa washarika na watu wote wenye mapenzi mema kwa Kanisa la Mungu, bila shaka mmekuwa mkiona na kusikia kupitia vyombo vya habari juu ya mgogoro unaoendelea katika KKKT Dayosisi ya Konde. Halmashauri Kuu baada ya kupokea taarifa ya Kamati Maalum kuhusu mgogoro huo ilizungumza na kukubaliana yafuatayo:

i. Halmashauri Kuu inatoa pole kwa waumini wote wa KKKT na wale wa Dayosisi ya Konde kwa kuumizwa na mgogoro huu ulioleta maumivu kwa Kanisa zima. ii. Halmashauri Kuu imeipongeza Kamati Maalum kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwapa pole kwa changamoto zote walizozipitia wakati wa kutekeleza wajibu huo waliokabidhiwa na Kanisa. Aidha; kamati imepongezwa kwa kuwa wavumilivu na watulivu wakati wote wa mgogoro.

iii. Halmashauri Kuu imezishukuru mamlaka za Serikali kwa jinsi wanashirikiana na Kanisa kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa wakati wote wa mgogoro.

iv. Halmashauri Kuu imejizuia kujadili au kuzungumzia kuhusu mambo yanayohusu mashauri yaliyopo Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya yanayohusiana na Mgogoro huu ili Kutoa nafasi kwa mamlaka hiyo utoaji haki kuendelea na utendaji wake kwa mujibu wa sheria za nchi.

v. Halmashauri Kuu imekemea na kuonya wale wote waliokuwa na wanaendelea kutoa taarifa zisizo za kweli na upotoshaji kuhusu mgogoro wa KKKT Dayosisi ya Konde. Katika hili, Halmashauri Kuu imepata nafasi ya kuwajadili baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu waliokwenda kinyume na mapatano yake. Wajumbe hao ni Askofu Dkt. Benson Bagonza wa KKKT Dayosisi ya Karagwe na Askofu Ambele Mwaipopo wa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, walioonekana kuwa mstari wa mbele katika kudharau mamlaka na maelekezo halali ya Kanisa, kutoa taarifa zisizo za kweli na upotoshaji kuhusu mgogoro huu na kuingilia kazi ya Kamati ya Kanisa.

Maaskofu hawa wamepewa nafasi ya kujieleza mbele ya Halmashauri Kuu. Baada ya kujieleza, Halmashauri Kuu imechukua hatua kadhaa dhidi ya viongozi hawa, na watajulishwa kwa maandishi juu ya hatua hizo. Ijulikane wazi kuwa hatua hizo ni kwa wajumbe hao binafsi kama wajumbe wa Halmashauri Kuu na sio kwa Dayosisi zao.

Pamoja na hatua hizo, Halmashauri Kuu imesikitishwa na baadhi ya Maaskofu wastaafu ambao wamejihusisha na kuingilia utendaji wa Halmashauri Kuu ya Kanisa. Hivyo, Halmashauri Kuu inatoa onyo kwa Wastaafu hao kuacha na kutorudia vitendo hivyo vya kwenda kinyume na maamuzi ya vyombo halali vya Kanisa. Halmashauri Kuu inawataka washarika wote wa KKKT na watu wote wenye mapenzi mema na Kanisa kuendelea kuliombea Kanisa la Mungu, ili liendelee kutekeleza wajibu wake wa kuendelea kuhubiri juu ya ufalme wa Mungu hapa duniani.