Habari kubwa ya gazeti la Upendo inahusu kauli ya viongozi wa dini waliozungumza na Upendo Media ambao wanaeleza kuwa na imani na Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Samia amechukua madaraka ya urais Ijumaa ya Machi 19 mwaka huu baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Hamis Juma kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Dk. John Magufuli.

Tunampongeza na kumtia moyo Rais wetu Samia. Hotuba aliyoitoa baada ya kuapa ilitoa mwanga tumepata kiongozi atakayejali utu, kuunganisha Watanzania na kuendeleza yale mazuri yaliyoasisiwa na hayati Dk. Magufuli.

Imani ya viongozi wa dini kwa Rais Samia inaongeza imani zetu kwake, yeye ni Rais wa kwanza mwanamke hapa Tanzania lakini ni mwanamke wa tatu kuwa Rais barani Afrika baada ya Liberia na Malawi.

Hongera Samia. Tunaunga mkono kauli za viongozi wa dini kuwa Rais Samia ataifikisha nchi kule inapotakiwa kufika, lakini zaidi ili hayo yawezekane tunamuhitaji zaidi Mungu na sisi pia kumpa ushirikiano.

Madaraka ya urais ndiyo makubwa katika nchi, hivyo kiti anachokalia Samia kinahitaji busara na hekima kubwa katika kuamua jambo lolote.

Mfalme Sulemani wakati alipoambiwa achague neno kwa Mungu, alimwomba Mungu ampe hekima. Ombi ambalo hata Mungu alistaajabia kwani hakukimbilia kuomba utajiri au maisha marefu. Ndiye mfalme aliyekuwa na hekima za kiwango cha juu ambazo alipewa na Mungu Mwenyezi.

Basi na sisi tuombe hekima zaidi kwa kiongozi wetu, ili aifikishe nchi kule kunapotakiwa. Tunaomba hivi kwa sababu wapo watu bado wana mawazo potofu kwa sababu tu anayeongoza ni mwanamke.

Askofu Alex Malasusa wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani alisema kuwa kinachoongoza siyo jinsia ya mtu, bali uwezo wake na ndiyo sababu wapo viongozi wanaume ambao walipata nafasi na waliharibu katika uongozi wao. Jinsia siyo kigezo cha kupima uwezo wa mtu.

Tunaamini kuwa Tanzania itaendelea kuwa salama katika mikono ya Samia Suluhu Hassan.