MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Fredrick Shoo amesema kuwa ushirikiano uliopo baina Kanisa hilo na chama cha Umoja wa Kiinjili wa Misioni (UEM), ni endelevu na umejikita katika nyanja za misioni na uinjilisti pamoja na kuunga mkono kazi za umoja wa Kanisa.

ASKOFU Dk. Shoo ameyasema hayo wakati wa kikao kilichowakutanisha kwa pamoja viongozi hao na kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Kanisa pamoja na kuongeza namna mbalimbali za ushirikiano uliopo baina ya KKKT na chama hicho cha Misioni (UEM).

Askofu Dk. Shoo alisema kuwa pia wanashirikiana katika kujengeana uwezo kwa viongozi wa Kanisa na kwamba wataendelea kuunga mkono kazi za umoja za Kanisa na tayari wametoa mchango mkubwa kuelimisha Wachungaji na Watheolojia katika Dayosisi za KKKT.

Katibu Mkuu wa UEM Mch. Dk. Volker Dally alisema kuwa KKKT ina umuhimu mkubwa katika chama hicho katika kuendeleza ushirikiano uliopo ni jambo la muhimu kwa ajili ya maendeleo ya sasa na miaka ijayo.

Alisema kuwa pamoja na kwamba UEM ina Dayosisi nne za KKKT ambazo ni wanachama wake lakini Kanisa hilo msharika wake na kila mara wamekuwa wakiangalia namna ya kuboresha namna ya kufanya kazi kwa pamoja katika programu mbalimbali na ndiyo sababu wanakutana ili kupata hatima nzuri ya ushirikiano huo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Kanda ya Afrika Mch. Dk. Ernest Kadiva alisema kuwa UEM imekuwa ikishirikiana na wadau wake katika kuleta maendeleo na kuhakikisha kuwa Injili inahubiriwa kwa usahihi wake, na pia kuwawezesha watumishi wa Mungu wanapata elimu ya kutosha juu ya Neno la Mungu na kuweza kufanya ya Mungu vizuri.