Viongozi wa dini walivyomllia Mungu kuhusu corona

NA ARAFUMANDE MUNUO

VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya dini waliitikia wito wa Serikali wa kuombea nchi na taifa, dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kushiriki Ibada ya maombi na toba katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Wakati wakiwasili viwanja hivyo, wote walizingatia kanuni zote zinazotolewa na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kujikinga na maambukizi kwa  kuvaa barokoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kutokaribiana (kukaa umbali za zaidi ya meta moja) na kutosalimiana kwa kushikana mikono.

Mgeni rasmi katika maombi hayo alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alieleza hali halisi ya maambukizi nchini Pamoja na hatua ambazo serikali imekuwa ikizichukua kukabiliana na ugonjwa huo ambao Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilishautangaza kuwa janga la dunia.

Maombi hayo yalitanguliwa na yale ya siku tatu ambayo yalitokana na wito wa Rais Dk. John Magufuli ya kuiombea nchi kwa siku tatu kuanzia Aprili 17 hadi 19 mwaka huu.

Wito wa Rais uliitikiwa na madhehebu mbalimbali huku baadhi ya viongozi wa dini waliozungumza na UPENDO wakisema kuwa ni neema kwamba Rais aliona umuhimu wa kuitisha maombi ya kitaifa kama sehemu ya hatua za kukabiliana na janga la ugonjwa huo.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kwa maombi hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba hali ya Tanzani bado ina unafuu tofauti na ilivyokuwa imetabiriwa na WHO.

Alisema shirika hilo lilikadiria kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili Tanzania ingekuwa na wagonjwa wa corona 524,776 (asilimia 80 wakiwa na dalili nyepesi na asilimia 15 wangehitaji uangalizi maalumu), lakini akasema hali bado ni tofauti.

Waziri Mkuu aliwaeleza viongozi wa dini kuwa pamoja na makadirio hayo ya WHO, bado Mungu amesimama na nchi ya Tanzania pamoja na Watazania wenyewe, kwani haijafikia idadi hiyo ya wagonjwa ambayo shirikia hilo lilikadiria.

Mpaka siku moja kabla ya maombi, Aprili 21, 2020 alisema Tanzania ilikuwa na maambukizi ya watu 184 huku watu kumi wakiripotiwa kupoteza maisha.

Alieleza kuwa jiji la Dar es Salaam na Zanzibar ndiyo maeneo yanayoongoza kwa kuwa na maambukizi mengi ikilinganishwa na maeneo mengine kutokana na idadi kubwa ya watu walioko katika maeneo hayo.

“Serikali inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti kuenea zaidi kwa ugonjwa huu, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya namna ya kujikinga na kuna kamati za kitaifa kwa ngazi mbalimbali zenye lengo la kufuatilia hatua kwa hatua za kuchukua za hali ya mgonjwa na kutoa mapendekezo yake kwa serikali,” alisema Majaliwa

Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, katika maombi hayo alisema pamoja na jitihada zote zinazofanywa na wanasayansi katika kutafuta tiba, lazima kumtanguliza Mungu kwanza.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema mwishoni mwa wiki kuwa wagonjwa 37 wa corona wameruhusiwa na kurejeshwa nyumbani.

Akizungumza kwenye hafla ya kupokea msaada wa sabuni na fedha kutoka kampuni ya Azania Group, alisema wagonjwa hao 37 ni kati ya wagonjwa 108 waliothibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona lakini hivi sasa hawana dalili zozote za ugonjwa kama homa, mafua na kikohozi.

“Watu hawa 108 hawana dalili zozote za ugonjwa kama vile homa au mwili kuchoka isipokuwa wapo katika vituo vya matibabu kusubiri vipimo vya mwisho ili kuthibika kwamba hawana virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kutoka vituoni, hivyo wamepona na wameruhusiwa kurejea nyumbani,” amesema.

Baadhi ya maombi

Askofu Dk. Malasusa aliomba hivi: “Mungu mtakatifu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Neno lako linatukumbusha kwamba wewe ndiye mwenye nguvu na msaada wetu, ndiyo maana watoto wako tumekusanyika mahali hapa kwa pamoja kama taifa la Tanzania popote wanaposikia hata kuona kwa pamoja, tunamimina miyo yetu kwako kukushukuru kwa kuwa wewe ni Mungu mwenye upendo hata unatuhurumia na kutusamehe makosa yetu yote.

“Tena ni Mungu ambaye unatukaribisha usemapo kupitia kitabu cha Nabii Isaya ‘njooni tusemezane’ na sisi Mungu tumekuja kukusihi kwamba katika dunia hata katika nchi yetu tumekabiliwa na tatizo hili la ugonjwa wa corona, Mungu tunakusihi ingawa tunaheshimu juhudi zote za wanasayansi lakini tunajua hata wao wameumbwa na wewe.”

Askofu Dk. Malasusa aliendelea kumuomba Mungu kwa kusema, “Ingawa tunaamini na kupokea dawa tunazopewa, lakini tunajua hata dawa zimeumbwa na wanadamu, hivyo Mungu tunakuita wewe usiyeshindwa na lolote uweze kushuka na kutamalaki katika nchi yetu  na hata katika ulimwengu ili Mungu tatizo hili liweze kuondoka.”

Askofu huyo pia alimuomba Mungu aondoe hofu na taharuki lakini alete umoja katika kipindi hiki na kutuwekea usikivu kwa maelekezo tunayopewa na walio katika utawala ili kupitia hayo tuweze kuondoka katika janga hilo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Mch. Bartholomeyo Cheyo alimuomba Mungu toba kwa ajili ya Tanzania na dunia nzima na kuomba rehema za Mungu.

“Tunakuja mbele zako kwa kujinyenyekeza na kutubu, Mungu mwenyezi utatusamehe na hili janga lililotupata dunia nzima, linatuhusu kila mmoja tunaona watu mbalimbali wakipata tatizo hili wakiwemo madaktari wanaotuhudumia Mungu tusaidie.”

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa'ichi  katika maombi yake alisema: “Kwa moyo wa imani tumaini na unyenyekevu  tunazielekeza sala zetu tukikuomba uyaangalie mateso yetu kutokana na maradhi haya ya ugonjwa wa corona, tunakuomba uyalinde maisha yetu uyaokoe wewe ndiye kimbilio letu na nguvu yetu.

“Tunakuomba uzibariki dawa wanazotumia wagonjwa waliopata maradhi haya na uwaponye, uwape uvumilivu na kinga madaktari wauguzi na wote wanaowatunza wagonjwa  na uwajalie wataalamu wetu wa afya, hekima, elimu na maarifa ya juu na utafiti sahihi wa tiba na chanjo sahihi ya maradhi haya,” aliomba Askofu Ruwa'ichi.

Askofu Ruwa'ichi, alisema pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa, waamini katika kuomba ndio njia pekee ya kushinda janga hilo la virusi vya Corona kwa kuwa Mungu aliwafundisha umuhimu wa kuomba.

Maombi mengine yametolewa na Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi, huku  jumuiya ya mabohora Tanzania ikiongozwa na mwenyekiti wake  Zainuddin Adamjee.

This news is from UPENDO, the weekly newspaper of ELCT Estern and Coastal Diocese.
Follow us on Facebook , Instagram and Youtube.