WACHUNGAJI wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT ), wamekumbushwa juu ya wajibu wa kuzilinda ndoa zao pamoja na familia zinazowazunguka. Wito huo umetolewa na Mch. Ebron Mwangomwile wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship la Muheza Tanga, wakati wa Kongamano la Wachungaji lililoandaliwa na wanawake wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste.

Kongomano hilo lilifanyika Kanisa la TAG la Michungwani Muheza Tanga “Ndoa ni mpango wa Mungu na wote tunalijua hilo, tuliambiwa kila mmoja wetu ataacha wazazi wake ataambatana na mwenzake nakuwa mwili mmoja, lakini sasa hivi imekuwa tofauti, unakuta tunawahubiria washiriki na kufundisha maadili, lakini katika familia zetu Wachungaji tumekuwa ni kongwa,” alisema.

“Wakati mwingine hata muda wa kuwa karibu na familia zetu ni mdogo sana, kwa hiyo unakuta tunashindwa kuwa waangalizi bora wa familia, mambo ya maadili yakianza kuharibika tunaanza kunyosheana vidole,” alisema.

Akinukuu 1Wakor 1-11 alisema kuwa ni lazima Wachungaji na Kinamama Wachungaji kuchukua muda mwingi wa kuombea ndoa zao na familia zao.

Naye Askofu Emanuel Ngairo Kutoka kanisa la EAGT alisema watumishi lazima wakumbuke kuwa Mungu ni lazima wadumishe upendo katika Makanisa wanayoyaongoza.