Umjue Askofu Dkt Alex Gehaz Malasusa
Askofu Alex Malasusa alizaliwa tarehe 18 April, 1961 katika kijiji cha Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya. Wazazi wake ni Mchungaji Gehaz Japhet Malasusa na Mama Subilaga Timoth Malasusa. Ni mtoto wa pili katika familia ya watoto nane.
Alisoma katika Shule mbalimbali za msingi kutokana na kuhama kwa wazazi. Mwaka 1976 alihitimu shule ya msingi Bungo Morogoro na baadae kujiunga na masomo ya Sekondari katika shule ya Kigurunyembe mwaka 1977. Baada ya masomo ya Sekondari alijiunga na Chuo cha Uongozi wa Biashara na baadae alijiunga na masomo ya uhasibu.
Alex G. Malasusa alifanya kazi katika mashirika mbali mbali likiwemo Shirika la Akiba la Taifa, kwa miaka minne na baadae kujiunga na masomo ya Theologia. Katikati ya masomo hayo, alipata fursa ya kusoma vyuo vingine vya nje katika mpango wa kubadilishana Wanafunzi. Alihitimu masomo mwaka 1995 na kubarikiwa kuwa Mchungaji katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani tarehe 03 Septemba 1995. Masomo na mafunzo mengine ni pamoja na Usimamizi na Utawala. Pia mafunzo ya dini mbali mbali.
Mwaka 1996 alifunga ndoa na Ericah Simon Nkonoki na kubarikiwa watoto watatu, Miriam, Michael na Mercy.
Askofu Alex Malasusa amefanya kazi Chuo Kikuu (DSM), Usharika wa Mburahati, Usharika wa Yombo, Usharika wa Msasani na kuwa Mkuu wa jimbo la Kinondoni (sasa Kaskazini). Pia Askofu amepata kuwa Msimamizi wa Kiroho (Chaplain) wa Seminari ndogo Kisarawe.
Askofu amekuwa:-
• Mkuu wa Kanisa KKKT kwa miaka 8 tangu 2007 hadi 2016 na Mkuu wa Chuo Kikuu Tumaini Makumira kwa kipindi chote.
• Pia amekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania CCT tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2017.
• Na sasa ni Mwenyekiti wa CCT – Dar- es- Salaam.
• Pia amekuwa makamu wa Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani. (LWF) kwa miaka 7 tangu mwaka 2012 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu WCC.
• Amekuwa Mwenyekiti wa PROCUMURA Tanzania kwa miaka sita.
• Amekuwa Mwenyekiti wa CSSC Tanzania kwa miaka minne.
• Kwa sasa ni Mwenyekiti wa CSSC kanda ya Mashariki.
• Ni Mwenyekiti wa bodi mbali mbali ndani na nje ya Kanisa.
Baadhi ya Vyuo Vikuu duniani vilivyomtunuku Shahada za Uzamivu za heshima za Udaktari:-
1. TRINITY LUTHERAN UNIVERSITY – USA
2. HELSINK UNIVERSITY – FINLAND
3. FINLANDIA UNIVERSITY – USA
Mstari wa Biblia anaoupenda ni:-
Yohana 3:30 ‘’Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua.’’