Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), imesema kuwa haitawabagua kwa namna yoyote wanasiasa ambao walishinda na walioshindwa katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni.

CCT imetoa kauli hiyo wakati wa kikao chake kilichofanyika katikati ya juma, Luther House jijini Dar es Salaam, yalipo makao makuu ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya KKKT.

Kikao hicho kilikuwa maalumu kwa ajili ya kuzindua mradi wa miaka mitatu wa utetezi wa haki za binadamu kupitia makanisa ya jumuiya hiyo na kuwajengea uwezo vijana.

Mbali na mradi huo pia Katibu Mkuu wa CCT, Canon Moses Matonya aliwaambia wawakilishi wa kikao hicho kuwa kupitia program hiyo, Kanisa litakuwa likifanya mapitio katika maeneo mengine ikiwemo nafasi ya Kanisa katika masuala ya kisiasa.

Kauli ya CCT imekuja siku ambayo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakila viapo vyao jijini Daodoma, tayari kuanza ngwe ya kuwatumikia wananchi katika majimbo yao. Canon Matonya alisema kwamba ni wakati ambao Kanisa linapaswa kuwaangalia upya waumini wake baada ya uchaguzi kwa sababu umepita na maisha lazima yaendelee.

Katika kikao hicho wajumbe walipata fursa ya kushauri Kanisa na kuangalia uchaguzi mkuu uliopita. Mwanasheria wa CCT, Glory Mafole aliwapitisha wajumbe hao wa kikao katika mtazamo wa jumla wa uchaguzi mkuu na kueleza kuwa mbali na changamoto zilizojitokeza, lakini aliipongeza Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa namna ilivyojipanga kuhakikisha zoezi linaenda vyema.

Wakizungumza katika kikao hicho, wajumbe walioshiriki walisema kuwa katika uchaguzi mkuu uliopita wapo ambao wamefurahi na wapo ambao hawajafurahi na kuwa hao wote wanapaswa waendelee na maisha.

Wajumbe hao kwa pamoja walikubali- ana Kanisa lazima lione haja ya kuhakikisha lina wakumbatia wote, waliofurahi, walioumizwa na wale ambao wameshindwa katika uchaguzi mkuu.

Mmoja wa wajumbe hao alisema; “Wapo wengi wanamaumivu na vilio wapo ambao wamekata tamaa, tuone haja ya kuangalia namna ambavyo tutawasaidia hao wote pamoja na wale ambao nao wamefanikiwa kushinda, kufanya hivyo ndio utume wa Kanisa tulioitiwa.”

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wakuu wa CCT wakiongozwa na Mwe- nyekiti, Askofu Alinikisa Cheyo ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania. Makamu Mwenyekiti wa Kwanza Askofu Dk. Frederick Shoo, Makamu wa Pili wa Mwenyekiti Dk. Jacob Chimeldya na Katibu Mkuu Canon Moses Matonya na Viongozi wa Baraza.

Kuhusu mradi uliozinduliwa, Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Utetezi, Clotilda Ndezi alisema mradi huo utawezesha CCT kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana kutoka shule za sekondari za kikanisa zipatazo 200.

“Tutaweza kuendesha program hii ili kuweka utetezi wa haki za binadamu kwa kutumia makanisa yetu, ni wakati mua- faka wa kuunganisha nguvu ya makanisa yetu ili kuweza kuinua haki za kijamii, maendeleo, usawa na kiuchumi,” alisema.

Alilitaja eneo la pili ambalo mradi huo utatekelezwa ni utoaji wa huduma za kishauri za kielimu, na ushauri nasaha na uhamasishaji wa makundi ya kijamii ili kuweza kuinua ari ya kila mmoja. Mwenyekiti wa CCT, Askofu Cheyo alisema kuwa program hiyo tayari imewekewa mpango mkakati mzuri wa kuweza kufikia shule za Kanisa ambazo ni za wanachama pamoja na walimu wake ili kuanza zoezi rasmi.

“Timu ya ufuatiliaji mpango imeandaliwa na mkakati ambao tumeuweka tumeimarisha Jumuiya iwe kitaifa, mpaka sasa kila mkoa na kila wilaya tunawawakilishi na tayari tumeshusha uwakilishi hadi ngazi ya vijiji ambapo Sharika na Mitaa yetu ya Kikanisa ipo,” alisema.

Naye Mchungaji Meja Daniels Mmari wa Kanisa la Jeshi la Wokovu ambalo ni moja ya makanisa wanachama alisema kuwa, mpango huo utainua ari ya vijana kwa kuwa ndani ya Kanisa wapo vijana waliokata tamaa.

“Sisi kama Kanisa ndio watu sahihi wa kuwaonesha njia vijana, tutawafikia kwa urahisi mahali walipo mashuleni na Makanisani ili kuwainua na kuwaganga mioyo waliokata tamaa na kuwaimarisha kuwa na fikra pevu za kujitegemea na kujiongoza,” alisema.