Mchungaji kiongozi wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Moivaro, Felix Moiro ametoa rai kwa Wakristo kuadhimisha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa kufanya mambo yanayompendeza Mungu badala ya kutumia siku hiyo kwa machukizo.

Mch. Moiro aliyasema Jumapili iliyopita, wakati akifundisha Neno la Mungu katika Ibada iliyofanyika Mtaa wa Machumba, unaotunzwa na Usharika wa Moivaro.

Alisema kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipokea Krismasi na Mwaka Mpya kwa mitazamo tofauti, kama vile kusherehekea kwa mavazi mapya pamoja na kupamba nyumba zao, huku wengine wakiichukulia Krismasi kuwa ya kwenda Kanisani na kutubu.

“Bwana Yesu yu karibu, tunavyosherehekea sikukuu hizi za Krismasi na Mwaka Mpya, Mkristo unapaswa kujifunza namna ya kusimama na kuwa karibu na Mungu wakati wote, tunapaswa kufanya maandalizi sahihi ya kumpokea Bwana Yesu na tunapaswa kumtwika mahitaji yetu kwa sababu yeye ndiye jawabu la mahitaji yetu,” alisema Mch. Moiro.

Pia alisema kuwa lazima Mkristo azifanye Krismasi na Mwaka Mpya kuwa siku za Ibada ndani ya mioyo yao na kuachana na starehe za kidunia, zisizompendeza Mungu ambazo hazina faida yoyote.

Alisema kuwa Wakristo wanatakiwa kuichulia Krismasi kuwa siku ya kusonga mbele kiroho, kwani aliyezaliwa ndiyo chanzo cha imani yao.

Akizungumzia kuhusu malezi kwa watoto, Mchungaji huyo alisema, wazazi na walezi wanapswa kuhakikisha wanawalea watoto vizuri na kuhakikisha wanawejenga katika imani waliyofundishwa ili iwe mbegu njema kwa jamii na Kanisa.

‘’Wazazi na Walezi mnapaswa kuwalea watoto wenu vizuri, kwa kuwafunza namna ya kusimama imara, kulishika Neno la Mungu na kuwalea katika maadili mema, ili Kanisa liwe imara lazima tuwalee vizuri watoto wetu. “Nyie wanafunzi leo mmebarikiwa msione kuwa mumefika, nyie bado ni watoto, yasikilizeni yaliyo mema na yenye kumpendeza Mungu na kusimamia imani, ili mafanikio yenu yalete baraka kwa Kanisa na jamii inayowazunguka pamoja na kwa wazazi wenu,’’ alisema Mch. Moiro.